BONDIA Bingwa wa Taifa wa kilo 59 toka Mkoa wa Tanga, Said Mundi “Smart Punch” amefiwa na baba yake, mzee Abdulrahman Mbaraka nyumbani kwake Zahrau mkoani Tanga. Kifo hicho kilitokea jana jioni muda mfupi kabla ya mpira wa Simba na Yanga. Imeelezwa kuwa sababu ya kifo hicho cha ghafla ni shinikizo la damu. Mauti yalimfika mzee Mbaraka akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali Bombo. Akielezea mtoto wa marehemu, Said Mundi alisema baba yake hapo awali hakuwa na ugonjwa huo lakini umekuja ghafla.
Said Mundi anaetegemea kupanda ulingoni Oktoba 26, 2012 kuzichapa na Bondia Jumanne Mohamed katika raundi 10, kugombea Ubingwa wa PST katika uwanja wa Mkwakwani-Tanga. Viongozi wote wa masumbwi wanaungana na Mundi katika wakati huu mgumu. Mungu ailaze roho ya mzee Abdi Mbaraka Mundi peponi – Amin