JK Atuma Rambirambi Vifo Ajali ya Mbeya

Dereva wa Mbunge akiwa katika gari la Wagonjwa wakisubiri ndege kuelekea Dar es Salaam kwa matibabu zaidi pamoja na Mbunge, Mary Mwanjelwa. Hawa ni miongoni mwa waliopata ajali ya lori la mafuta jana. Picha kwa hisani ya Mbeya Yetu Blog.

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amewatumia salamu za Rambirambi Wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Shinyanga kufuatia ajali zilizotokea Oktoba 2, 2012 mikoani humo kwa nyakati tofauti. Katika salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro kufuatia ajali iliyotokea katika Mlima Mbalizi, Barabara Kuu ya Mbeya /Tunduma, ambapo watu wapatao kumi na mmoja (11) wanasadikiwa kupoteza maisha na wengine ishirini na moja (21) kujeruhiwa.

Ajali hii inasadikiwa ilihusisha lori la mafuta kugonga magari mengine matatu ya binafsi na kusababisha moto ambao umeteketeza watu na mali.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa, habari za ajali za kusikitisha za ajali mbaya mkoani mwako” Rais amesema na kumuambia Mkuu wa Mkoa “Nakupa pole kwa ajali hiyo ambayo imesababisha msiba mkubwa mkoani mwako na kuleta simanzi na huzuni kubwa, sisi sote tumehuzunishwa na kushtushwa” amesema.

Katika salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Nassoro Rufunga kufuatia ajali iliyotokea Kahama, ambapo watu watatu (3) wamefariki na wengine ishirini na tatu (23) kujeruhiwa ambapo inasemekana basi la abiria liligongana na lori la mizigo.

Rais amewaomba Wakuu wa Mikoa kuwafikishia salamu za rambirambi ndugu wa marehemu na pia kuwatakia heri majeruhi wote ili waweze kurudi katika shughuli zao za maendeleo.
Rais ametuma salamu hizo akiwa anatarajia kuanza ziara ya kiserikali nchini Kanada kuanzia tarehe 3-6 Oktoba, 2012 kufuatia mualiko wa Gavana Jenerali wa Kanada Mheshimiwa David Johnston.

Katika salamu zake, Rais pia amewataka viongozi wote kutochoka kuwakumbusha raia, wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva kuwa waangalifu na makini wakati wanapokuwa safarini kwani usalama barabarani ni jambo muhimu sana wakati wanapokuwa barabarani.

Rais ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja wapo kuhakikisha usalama wa kila mtumiaji unazingatiwa, na ni jukumu la ziada kwa madereva wanaoendesha vyombo hivyo. Rais pia amewakumbusha madereva wote nchini kuwa makini na magari yao na pindi wanapokuwa barabarani.

“Nawaomba viongozi wote tusichoke kuwakumbusha madereva na wananchi kwa ujumla kuwa usalama barabarani ni usalama wa maisha na mali zao, hivyo wote wanatakiwa kuwa makini wakati wote.”
Rais amekumbushia kuwa sherehe za siku za usalama barabarani zisiwe zinaazimishwa na kusahaulika siku hiyo hiyo, ziwe za kudumu na siku zote wananchi, wamiliki wa vyombo vya moto, na madereva watambue kuwa usalama barabarani ni kitu cha kudumu, hivyo sheria na taratibu zinafaa kuzingatiwa siku zote, ili kujiepusha na vifo, ulemavu na uharibifu wa mali.

Rais Pia amewataka wakuu wa vyombo vya Usalama nchini kufanya uchunguzi wa vyanzo vya ajali hizi, kuwafikisha mbele ya sheria na kuwachukulia hatua wale wote watakaokuwa na hatia na kusababisha uharibifu huu mkubwa wa maisha na mali za watu.