Matajiri Wakubwa Duniani Waichangia Tanzania Kusaidia Uzazi Salama

Bendera ya Tanzania

Na Mwandishi Maalumu, New York, Marekani

MATAJIRI wawili wakubwa duniani Oktoba 2, 2012, wameichangia Tanzania kiasi cha sh. bilioni 24.1 (sawa na dola za Marekani milioni 15.5) kwa ajili ya kuendeleza afya ya akinamama na kusaidia uzazi salama hasa katika maeneo ya vijijini.
Matajiri hao, Michael Bloomberg ambaye ni Meja wa Jiji la New York, Marekani na Mama Helen Agerup wa Sweden, wametangaza mchango wao huo mkubwa kwa Tanzania kwenye mkutano maalum wa waandishi wa habari uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Pamoja na matajiri hao kwenye mkutano huo wa waandishi wa habari walikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Kati ya fedha hizo, Meya Bloomberg wa Jiji la New York lenye wakazi milioni 8.4, anatoa kiasi cha dola za Marekani milioni nane kupitia Taasisi yake ya Bloomberg Philanthropies wakati Mama Agerup anatoa kiasi cha dola milioni 7.5 kupitia taasisi yake na mumewe ya H&B Agerup Foundation.
Meja Bloomberg amekuwa anasaidia afya ya akinamama na juhudi za uzazi salama katika maeneo ya vijijini katika Tanzania tokea mwaka 2006 wakati hii itakuwa mara ya kwanza kwa Taasisi ya H&B kuungana na Bloomberg Philanthropies kusaidia sekta ya afya katika Tanzania.
Akizungumza kwenye shughuli hiyo muhimu, Meya Bloomberg amesema kuwa yeye na taasisi yake wameamua kuendelea kuunga mkono jithada za Tanzania katika kuinua afya ya akinamama na kupunguza vifo vya uzazi kwa sababu ya matokeo mazuri ambayo yamepatikana tokea Bloomberg Philanthropies ianze kuunga mkono jitihada hizo za Serikali mwaka 2006.
Amesema kuwa taasisi yake inajihusisha katika maeneo mawili makubwa. Eneo moja ni kujenga na kukarabati vituo vya afya na zahanati katika maeneo ya vijijini na pili ni kutoa mafunzo kwa watu wasiokuwa watalaam wa afya pamoja na wakunga kuweza kusaidia uzazi salama vijijini. Mpaka sasa taasisi hiyo imefundisha kiasi cha watu 106 kuweza kufanya kazi ya uzazi salama na ukunga chini ya msaada wake kwa Tanzania.
“Tunaona matokeo ya kuvutia sana. Hata kama idadi ya akinamama wanaopoteza maisha haijawa ya chini –akinamama 13 kati ya 1,000- kama ile ya Marekani lakini dhahiri kuwa idadi inapungua kwa kiasi cha kutia moyo”.
Ameongeza Meja Bloomberg: “Zaidi tunaifanya kazi hii katika Tanzania kwa sababu tunashughulika na Rais Kikwete, kiongozi mbunifu, kiongozi mkweli na muadilifu, kiongozi mchapakazi na anayetaka kuonyesha tofauti katika maisha ya wananchi wake.”
Naye Mama Helen Agerup amesema kuwa alitembelea Tanzania mwaka jana baada ya kushawishiwa na binti yake ambaye alikuwa ametembelea Tanzania mapema na kuvutiwa na jitihada za Serikali na zile za Taasisi ya Bloomberg kuhusu afya ya akinamama.
“Nilivutiwa sana na kazi inayofanywa na Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Bloomberg kuzuia vifo vinavyosababishwa na mambo yanayoweza kuzuilika yaani kutokwa damu kupita kiasi na magonjwa ya kuambukiza kutokana hasa na tatizo la ukimwi,” amesema mama huyo.
Naye Rais Kikwete ameshukuru sana Meya Bloomberg na Mama Agerup akisema kuwa misaada yao inaleta tofauti kubwa katika afya za akinamama katika Tanzania.
“Katika nchi ambako uwiano wa daktari mmoja na wagonjwa ni daktari mmoja kwa wagonjwa 30,000 na mganga mmoja kwa wagonjwa 23,000 na ambako akinamama waja wazito wanatembea zaidi ya kilomita tano kwenye uchungu, misaada ya namna hii ni muhimu sana kwa nchi yetu. Tunawashukuru sana.”
Amesema kuwa umuhimu wa kuboresha afya ya akinamama ni moja ya maeneo ya kipaumbele cha Serikali na hali hiyo itaendelea mpaka tatizo la vifo vya uzazi litakapopungua sana.