Na Onesmo Ngowi
MASUMBWI au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea….!
Mabondia wengi na walio mabingwa wa dunia huajiri “cutman” kwa kipindi chote cha maisha yao ya ngumi. Kutokana na umuhimu wa kumhudumia bondia wake vizuri ma-cutman wengi wanalipwa fedha zaidi ya madaktari katika mpambano.
Katika mpambano wa ngumi kuna washika vibao (Card Girls) vinaoonyesha raundi inayofuata. Mara nyingi watu hawa huwa ni wasichana wanamitindo au waliobobea kwenye majukwaa kama wanamuziki, wanamitindo, wacheza shoo n.k. Kila raundi inapoisha mshika kibao huingia kwenye ulingo akitembea kwa maringo na kuonyesha raundi inayofuata.
Mara nyingi mwendo wake husaidiwa na musiki mororo unaopigwa na watazamaji hufuatilia kwa makelele ya furaha. Wapo vile vile washika vibao ambao ni wanaume wanaofanya mazoezi ya kutunisha musuli na haswa mpambano wenyewe unapokuwa ni wa wanawake. Vile vile kuna mtangazaji (Commentator) ambaye anatakiwa kutangaza mpambano wenyewe. Mtangazaji wa mpambano hutangaza mpambano wenyewe kwa ujumla akianzia na aina ya mpambano, wageni waliohudhuria na mabondia wahusika.
Pengine ni wakati anapotangaza mabondia husika ndipo anapotakiwa kutumia madoido ya hali ya juu kumnadi kila bondia. Kazi yake nyingine ni kutangaza matokeo ya kila mpambano haswa inapozingatiwa kuwa mchezo wa ngumi unajumuisha mapambano mengi madogo madogo (supporting bouts) kabla ya mpambano mkubwa. Waliotajwa hapo juu ndio wahusika muhimu mbali na promota na meneja kuendesha pambano la ngumi.
MIFUMO YA NGUMI NA MADHARA YAKE KWENYE MAENDELEO YAKE
Mifumo ya ngumi imekuwa inabadilika na wakati, tangu ngumi zilipoanza. Lakini nitaanzia na hapa kwetu Tanzania. Ipo mifano mingi inayoonyesha namna mabondia wetu wa kitanzania walivyo na uwezo mdogo wa maswala ya ngumi. Mfano mmoja ni jinsi Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) ilivyokwisha jitahidi kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuwawezesha baadhi ya mabondia kushindania tuzo mbalimbali za kimataifa. Kana kwamba ni kazi ta TPBC kuhakikisha kwamba bondia bingwa wa tuzo hizi kuzitetea, mabondia hawa wanaishia kupoteza mataji yote waliyoyashinda kwa gharama kubwa na juhudi hizi za TPBC bila kuyatetea.
Baadhi yao wakitumiwa na wababaishaji wachache wanaojiita mameneja feki wanaodiriki hata kuushutumu uongozi wa TPBC kwamba uliuuza mikanda yao ya ubingwa. Kuna usemi wa kiswahili unaosema kwamba “akutukanaye hakuchagulii tusi”. Ni kioja cha hali ya juu tena dhihaka isiyo na upeo kwa mtu kusema kwamba mkanda wake umeuzwa. Mkanda wa bondia ni mali yake na haiwezekani tu mtu akajitokeza barabarani amevaa mkanda wa ubingwa asiokuwanao. Kufanya hivi ni sawa na mtu kuvaa nguo za askari wa zima moto na kwenda nazo disko.
Dhihaka kama hizi na nyingine nyingi zilnaufanya uongozi wa TPBC uachane na kujishughulisha na maswala ya kupromoti na kumeneji. Kwa kuwa juhudi zake za kuwasaidia mabondia pale ambapo mapromota na mameneja hawakuwepo zinachukuliwa kama njia mbadala ya kujinufaisha kifedha, iliamua kukoma. Mikanda ambayo TPBC iliigharamia ili kuhakikishia mabondia wa kitanzania wanayashinda ni pamoja na IBF/Afrika, CBC, ECAPBF na WBU.
Ni vizuri nieleze tu kwamba bondia anayeshinda mkanda wa ubingwa anatakiwa awe ameutetea katika kipindi kati ya miezi minne na mwaka mmoja (Division ndogo kuanzia Light Fly mpaka Super Light Weight wanatakiwa wawe wametetea katika kipindi cha miezi sita, Kunzia Welterweight mpaka Heavyweight anatakiwa awe ametetea katika kipindi cha mwaka mmoja husuan ubingwa wa dunia).
Mashirikisho mengi madogo mbali na IBF, WBA, WBO na WBC hayana sheria ngumu zinazomtaka bondia atetee ubingwa wake katika kipindi hiki kilichotajwa hapo juu. Hivyo huwapa muda kati ya miezi sita mpaka mwaka mmoja an wakati mwingine bondi anakaa tu na mkanda mpaka atakapojitokeza bondia mwingne anayeutaka.
Lakini mashirikisho kama IBF, WBC, WBO na WBA ni lazima bondia bingwa acheze na bondia anayemfuata kwenye viwango katika kipindi kilichotajwa cha miezi sita kwa ubingwa wa bara (Continental) mpaka mabara (Intercontinental). Sheria za mashirikisho haya zimeufanya mchezo wa ngumi kuwa na upinzani wa hali ya juu. Bingwa anapotakiwa kutetea ubingwa na bondia anayemfuata kwenye viwango na kwa muda uliotakiwa kunaufanya mchezo wa ngumi kuwa na upinzani wa hali ya juu.
Bondia anaposhindwa kutetea ubingwa wake katika kipindi hiki hunyanganywa ubingwa na kutangazwa kuwa ubingwa wenyewe uko wazi. Ubingwa uliotangazwa kuwa wazi unawafanya mabondia walio namba moja hadi nne kucheza mapambano ya mtoano (Elimination Titles) ili kuwapata mabondia wawili watakaoshindania ubingwa. Kwa ajili ya upinzani na malipo mazuri mapambano yote ya mashirikisho haya hutangazwa kwa njia ya tenda (bidding). Mapromota wanatakiwa watume ofa ya fedha watakazolipa mabondia na atakayetoa donge nono ndiye anayeshinda katika tenda ya kupromoti pambano husika.
Kwa wenzetu inakuwa rahisi kwani mifumo yao wa kupromoti ngumi inamruhusu promota kuweza kukubaliana na makampuni mbalimbali ya mitandao ya televisheni itakayomlipa fedha za kupromoti. Anapopiga mahesabu yake na kuona kuwa anazo fedha za kutosha na faida ndipo anapotuma tenda yake. Iaendelea…!
Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com