Na Mwandishi Wetu, Hai
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linawashikilia watu saba kutoka Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za kujiunganishia umeme kinyume cha sheria, hali ambayo imekuwa ikilisababishia shirika hilo kupoteza mapato mengi kutokana na wizi wa umeme.
‘Matapeli’ hao wamekamatwa katika Operesheni ya Kamata wezi wa umeme Tanzania inayoendelea nchi nzima, iliyoendeshwa na TANESCO mkoani Kilimanjaro maeneo ya Masama, Machame na Kia wilaya ya Hai lengo likiwa ni kutokomeza tatizo la wizi wa umeme ambalo limeonekana kushika kasi mkoani hapa.
Akizungumza Meneja wa Tanesco wilaya ya Hai na Siha, James Chinula alithibitisha kukamatwa kwa watu hao na kusema kuwa, wilaya ya Hai ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa na wezi wengi wa umeme. Chinula alisema kumekuwepo na watu ambao wamekuwa wakijiundia nyaya kwenye miundombinu ya umeme kinyume cha taratibu, jambo ambalo ni hatari sana kwa usalama wa wananchi wanaoishi maeneo hayo.
“Operesheni ya kamata wezi wa umeme Tanzania inayoendeshwa nchi nzima, ni endelevu kwani kumekuwepo na watu ambao wamekuwa wakijiunganishia umeme kinyemela kinyume cha sheria jambo ambalo ni hatari na hutusababishia kupata hasara,” alisema Chinula.
Aidha alisema kumekuwepo na madhara mengi yatokanayo na kujiunganishia umeme kinyume cha sheria ikiwa ni pamoja na watu kupoteza maisha kutokana na kukosekana kwa tahadhari na umakini katika uwekaji nyaya hizo. Alisema wananchi wengi ambao huiba umeme hutegesha nyaya ardhini pasipo kujali madhara wala hasara ambazo zinaweza kutokea ambapo wananchi wengi wakiwemo watoto wameripotiwa kupoteza maisha baada ya kukanyaga nyaya hizo.
Kutokana na hali hiyo, Chinula aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuiba umeme na badala yake kwa wale wote wanaohitaji umeme kufika ofisi za Tanesco ili kuweza kuunganishiwa kihalali na kuondokana na tabia ya kulihujumu shirika. Watu hao waliokamatwa ni Ally Omary, Stephano Eliafiye, Elia Salimo, Yohana Zacharia, Anold Jonas, Shaningwansia Ulomi na Sharifa Ally wote wakazi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambapo walijiunganishia umeme kinyume cha sheria.