WASANII wamepewa changamoto ya kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni yao juu ya uundaji wa Katiba mpya ili fani yao iweze kutambulika kisheria.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Idara ya Mfuko wa Uwezeshaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Charles Malimba wakati akitoa mada kuhusu Sanaa ya Utamaduni na dhana ya Tasnia ya Ubunifu inavyoweza kuleta ajira kwa vijana wa Tanzania katika Tamasha la 31 la Sanaa na Utamaduni linaloendelea kwenye uwanja wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni(Tasuba), Bagamoyo, mkoani Pwani.
Alisema kuna haja ya wasanii kujitokeza katika kutoa maoni juu ya Katiba mpya ili itambuena kutoa kipaumbele mambo mbalimbali katika sekta ya sanaa na utamaduni.
Aidha Malimba aliongeza kuwa wakati umefika kuwa Katiba itamke sanaa na utamaduni kazi , pia kuwepo na viwango vya malipo kisheria kwa kuwa sekta hiyo inavyoweza kuchangia mapato kwa serikali.
Malimba alitaka vyuo vinavyofundisha sanaa utamaduni nchini kutunza kumbukumbu za fani hizo na kuurithisha ili kuepusha kupotea kwa utamaduni wa Mtanzania , huku akiwataka wanafunzi wa fani hizo kusoma kwa bidii na kuitekeleza ili kuweza kuwasaidia wengine na kuifanya sekta hiyo kuwa ajira.
Naye mhitimu wa chuo hicho wa mwaka 2010, Nyenyembe Jacoub na Baraka Matitu walisema ili kuweza kukuza sanaa na utamaduni kuna umuhimu wa kuanzisha shule maalum kuanzia chekechea hadi elimu ya juu.
Akijibu hoja hiyo, Malimba alisema ni changamoto kwa wadau mbalimbali binafsi kuanzisha shule hizo kama ilivyo kwa zingine kwa kuwa suala hilo halina kipingamizi, huku akisisitiza suala la utunzaji wa sanaa na utamaduni ni wajibu wa kila wanajamii.
Baadhi ya wasanii waliomba serikali iweke mikakati ya kuweza kuwasaidia wasanii hususan wale wachanga ili kuweza kukuza vipaji vyao, kwa kuwa vingi vinaanzishwa lakini vinashindwa kuendelea kwa kukosa wafadhili.