RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Septemba 27, 2012, amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates, Bi. Melinda Gates. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Club House, kwenye Hoteli ya Ngurdoto, mjini Arusha, Rais Kikwete na Bi. Gates wamezungumzia masuala mbalimbali na hasa kuhusu jinsi taasisi hiyo inavyoweza kuisaidia Tanzania hasa katika maeneo ya kilimo na afya ya akinamama.
Rais Kikwete amemwomba Bi. Gates kuangalia jinsi ya kuisaidia Tanzania kuanzisha taasisi ya kufutilia utekelezaji wa mipango, program na maamuzi yote ya Serikali kuhusu mageuzi ya kilimo katika Tanzania.
“Tuna mambo mengi na shughuli nyingi zinazoendelea katika sekta ya kilimo. Tunafanya mengi, lakini lazima tuwe na uwezo wa kujua kila jambo linalofanyika liko kwenye hatua gani na linakwenda kwa mafanikio ama matatizo yapi,” amesema Rais Kikwete.
Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation inasaidia taasisi ya namna hiyo katika Ethiopia, nchi ambayo kilimo chake kinakua kwa asilimia sita kwa mwaka. Naye Bi. Gates amemwambia Rais Kikwete: “Kama hilo ndilo jambo mnalolitaka basi hakuna shaka kuwa sisi tutavutiwa na jambo hilo.”
Bi. Gates yuko mjini Arusha kuhudhuria Mkutano wa Pili wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani katika Afrika (AGRA) ambao umefunguliwa leo na Rais Kikwete kwenye Hoteli ya Ngurdoto. Akizungumza kwenye sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo, Bi. Gates amemwagia sifa Rais Kikwete akimweleza kama kiongozi anayejali sana maslahi ya Tanzania na maslahi ya Afrika.
Bi. Gates amesema kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza ambayo yeye na mumewe, tajiri Bill Gates walitembelea miaka 19 iliyopita na tokea wakati huo wameitembelea nchi hiyo mara nyingi zaidi kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika. “Hata mwaka huu, hii ni mara yangu ya pili kuja Tanzania.”
Ameongeza: “Naipenda na kuitembelea Tanzania siyo tu kwa sababu watu wake ni wema na wakarimu sana, na wala siyo tu kwa sababu nchi yenyewe inavutia sana, lakini hasa hasa kwa asababu Tanzania ni mfano usiokuwa na kipimo wa maendeleo na inajali sana mtu ambaye nasi tunamjali sana – mkulima.”