Wasanii wa Sanaa za Maonesho Wapewa Changamoto Bagamoyo

Baadhi ya sanamu zilizochongwa na wasanii.

Na Magreth Kinabo -Maelezo, Bagamoyo

WASANII wa sanaa za maonesho nchini wamepewa changamoto ya kutambua kuwa watalii ni hadhira ambayo wanaweza kuilenga katika ubunifu wa kazi zao ili kukuza utalii wa kiutamaduni, ambao utasaidia kuongeza mapato kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TAsuBA), Juma Bakari wakati akiwalisisha mada ya ‘Sanaa za Maonesho kama Kivutio cha Utalii Tanzania’ kwenye Kongamano la Tamasha la 31 la Sanaa na Utamaduni lililofanyika Uwanja wa Taasisi hiyo iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Alisema sanaa za maonesho ni kivutio kikubwa cha utalii hivyo kuna kila sababu ya wasanii kuwa na mtazamo huo ili kuangalia fursa zilizopo. Alisema wasanii lazima watambue watalii ni hadhira ambayo wanaweza kuwalenga kwa kuwafahamu kwa makundi.

Alitolea mfano kuwa katika kipindi cha mwaka 2005 sekta ya utalii imeingiza mapato makubwa na imekuwa chanzo cha mapato ya fedha za kigeni,ambapo nchi yetu ilipata dola za Marekani bilioni 1.8 na inatarajia kupata dola za Marekani bilioni tatu ifikapo mwaka 2015.

Aliongeza kuwa ni vizuri wasanii hao wakajifunza kutoka kwa wenzao wa Kenya na Uganda ambao wamefanikiwa kuhamasisha utalii huo kwa kutumia ngoma na muziki wa asili. Mkuu huyo wa taasisi hiyo alisema Lugha ya Kiswahili inaweza kuwa ni kivutio cha watalii ikiwa wasanii hao watatayarisha tamthilia za lugha kwa maneno mepesi.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazowakabili katika kukuza utalii huo, alisema zaidi ya vikundi 4000 vilivyosajiliwa, hakuna hata kimoja kinachoonyesha kukuza utalii huo. Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa elimu ya biashara na ujasiriamali hali inayosababisha vikundi vingi kutegemea wafadhili hatimaye kuanzishwa halafu vinakuwa havipo.

Aidha alifafanua kuwa kampuni za kitalii nazo zinachangia kutokuza utalii huo kwa kuwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili za mwaka 2011-2012 kampuni hizo ziko 385, kati ya hizo 85 ni za kigeni . Pia kulingana na utafiti uliofanywa hata zilizobakia zinaendeshwa na wageni ambao sio jambo rahisi kwa wao kuukuza kwa vile hawaufahamu.