Wadau Waibana Serikali Kuhusu ARV Bandia

Baadhi ya dawa za ARV

BARAZA la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA), limeitaka Serikali kuwaeleza wananchi madhara watakayoyapata baada ya kutumia dawa bandia za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV), ambazo zimesambaa katika maeneo mbalimbali nchini. Mbali na hilo, wameitaka ikiri uzembe ambao umejitokeza katika utaratibu wa kuagiza, kununua, kusambaza na kuzigawa dawa hizo kwa watumiaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji wa NACOPHA, Deogratius Peter alisema Serikali inapaswa kutoa ufafanuzi wa kina juu ya hali ya baadaye ya watu ambao walikuwa wanatumia dawa halali kisha wakatumia bandia.

Peter alisema Serikali inawajibika kuwasaka wahusika wa kashfa hiyo na kuwachukulia hatua kali za kisheria, vinginevyo watumiaji wa dawa hizo watapoteza matumaini na kuvuruga juhudi za taifa za kukabiliana na maambukizo ya Ukimwi.

“Kupitia NACOPHA tunaitaka Serikali itoe elimu na taarifa sahihi ili watumiaji wapate uwezo wa kuzitambua zipi ni dawa bandia na zipi ni halali,” alisema Peter.

Alisema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo la dawa bandia, Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kwa kuanzisha utaratibu wa watumiaji wa dawa hizo kuzirejesha kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya na kutolewa kwa dawa halisi.

“Tiba hii ina kiambatanisho kimoja tu, wakati tiba kamili ina viambatanisho vitatu, hii ndiyo iliyopitishwa na Serikali itumike hapa nchini,” alisema Peter.

Alisema NACOPHA inaendelea na uchunguzi ili kubaini idadi halisi ya mikoa ambako dawa hizo zilifika mbali ya Dar es Salaam, Mara na Tanga ambako Serikali ilikiri kuwa zilifika. Kauli hiyo ya NACOPHA inakuja siku chache baada ya Mkuu wa Idara ya Dawa katika Kitengo cha Ukimwi, Hospitali ya Amana, Dar es Salaam, Charles Lyimo kuitaka Serikali kujichunguza yenyewe kwa kuwa dawa hizo hazisambazwi na watu binafsi.

“Siyo rahisi kujua kwamba hii ni dawa halisi au bandia, lakini tuna uhakika na dawa tunazotumia kwa sababu zinaagizwa na Serikali peke yake. Hakuna mtu binafsi aliyepewa tenda (zabuni) ya kuziagiza. Inapeleka oda kiwandani na ndiyo inayozigawa dawa hizo na kuzisambaza kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Lakini pia dawa hizi zinatengenezwa Arusha kwenye kiwanda kilichopewa kibali na Serikali. Kama kuna dawa bandia, basi Serikali ijihoji… Tangu sakata hili limeanza, wizara inajigongagonga tu… hawatuhusishi wala kutuuliza… na sisi tunaendelea tu kugawa dawa…”

Awali, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilisema haijajua kiasi halisi cha dawa hizo zilizoingia sokoni, lakini ikisisitiza kwamba athari zake ni kidogo huku Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ikibaini makopo 1,360 ambayo yako mikononi mwa wagonjwa.