Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es Salaam
SERIKALI imewataka wananchi kutopuuza taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kuhusu athari za mvua kubwa zinazotarajia kunyesha nchini kuanzia Oktoba mpaka Desemba 2012 na kuwataka wanaoishi mabondeni kuhama ili kuepuka madhara ya kukumbwa na mafuriko.
Hatua hiyo imekuja kufuatia baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni hususani jijini Dar es Salaam kuupuuza taarifa za wataalam na kukaidi maagizo yanayotolewa na viongozi wa serikali ya kuwataka kuhama katika maeneo yenye mikondo ya maji na yale yaliyoainishwa kuwa hatari kwa maisha ya binadamu.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha kamati ya maafa ya mkoa wa Dar es Salaam kilichowahusisha wakuu wa wilaya za Temeke, Ilala, Kinondoni pamoja na wataalam wa sekta ya Afya, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Zimamoto na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam mwenyekiti wa kikao hicho na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema uongozi wake unajipanga kuhakisha kuwa wananchi wanapewa elimu ya namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali.
Amesema Kamati ya Maafa Mkoa wa Dar es Salaam imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa shughuli za uokoaji pindi majanga yanapotokea zinafanyika kwa ufanisi na kuweka nguvu kubwa katika kuwasaidia wananchi kabla ya tatizo kutokea badala ya kujikita katika kuokoa wakati wa maafa.
Mwenyekiti amezitaka manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni kuhakikisha kuwa zinatenga maeneo mbadala kwa ajili ya kupeleka na kuhifadhi watu yanapotokea mafuriko na kuwataka kutotumia maeneo ya shule kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika.
“Natoa agizo kwa viongozi wa manispaa kutenga maeneo mbadala ya kuhifadhi waathirika wa majanga mbalimbali ili shule ziendelee kutumika kama mahali pa watoto kujifunza, hata kama shule zimefungwa lazima tutafute maeneo mbadala haiwezekani tufunge shule wakati maeneo yapo ya kutosha”
Amesema kuna tabia ya baadhi ya waathirika wanapopewa msaada wa kuhifadhia katika maeneo ya shule huyatumia kinyume cha utaratibu na wakati mwingine kuharibu miundombinu na wakati mwingine kugoma kuondoka na kukwamisha shughuli za uendeshaji wa shule.
Aidha ameitaka Kamati ya Maafa Mkoa wa Dar es Salaam kufuatilia mahitaji muhimu ya misaada yatakayokua yakitolewa wakati wa majanga ili kuwa na akiba na kuepuka usumbufu unaojitokeza wakati wa tatizo na kuziagiza halmashauri kupitia kwa wakurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya kununulia vifaa vya uokoaji vitakavyotumika pindi yanapotokea majanga.
‘’Lazima tuwe na ufahamu kutambua yatakayotokea kwa maana ya kujenga uwezo wa madawa, vifaa vya vya kisasa vya kuokolea yanapotokea mafuriko,kutenga maeneo maalum na vyumba vya kuuguzia wagonjwa waliopata madhara mbalimbali,” amesema.
Sadiki amewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya mtaa kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kufanya usafi na kuzibua mifereji na kuepuka kutupa taka ovyo ili kurahisisha maji kutiririka kutoka eneo moja hadi jingine bila kikwazo chochote.
Kwa upande wake wake Dkt. Meshack Shimwela kutoka hospitali ya manispaa ya Ilala amefafanua kuwa kufuatia kuongezeka kwa majanga mbalimbali yanayotokana na vitu vya asili na vile vya kutengeneza imeundwa timu maalum ya kukabiliana na dharula (DAR MAERT).
Amesema utoaji wa huduma kwa waathirika wa majanga mbalimbali umekua ukikabiliwa na changamoto za ukosefu wa fedha, wataalam na vifaa vya kutosha hasa pale yanapotokea maafa makubwa.
Naye mganga mkuu wa hospitali ya Amana Dkt. Christopher Mzava akieleza kwa wajumbe kuhusu mkakati wa kukabiliana na mafuriko amesema kuwa suala la utupaji wa taka na uchafuzi wa mazingira limekua chanzo cha kuchangia kuziba kwa mifereji inayosafirisha maji kuelekea baharini hasa katika jiji la Dar es Salaam. Alisema licha ya changamoto za kukosekana kwa vifaa vya uokoaji vya kutosha zikiwemo ndege maalum (Helikopta) jamii inahitaji kuelimishwa kuhusu namna bora ya kukabiliana na kukwepa majanga.
Kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo mkoa wa Dar es salaam umeshuhudia majanga mbalimbali yakiwemo milipuko ya mabomu ya Mbagala iliyotokea mwaka 2009, milipuko ya mabomu ya Gongolamboto 2012 na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2011 na kusababisha upotevu wa maisha, mali na uharibifu wa miundombinu.