Mabondia Bingwa Uzito wa Kati Tanzania na Uganda Kupambana

Rais wa TPBO Yassin Abdallah -Ustaadh (kushoto) akitiliana saini na bondia Thomasi Mashali ikiwa ni sehemu ya malipo ya awali kwa ajili ya maandalizi ya mpambano wake wa kugombania Ubingwa wa Afrika Mashariki.

Bondia kutoka nchini Uganda, Med Sebya

Na Mwandishi Wetu

BONDIA Bingwa uzito wa kati (middle) kg 72.5 wa nchini Uganda, Med Sebyala (Bingwa Uzito wa Kati Uganda- UPBC) na Bingwa wa uzito huku kutoka nchini Tanzania, Thomas Mashali (Bingwa Uzito wa Kati Tanzania -TPBO), Oktoba 14 wanatarajia kupanda jukwaani kumtafuta mbabe wa uzani huo. Pambano hilo linatarajia kuwakutanisha mabondia wakali na wakatili wawapo ulingoni kwa Kanda ya Afrika Mashariki.

Bondia Sebyala kutoka Uganda na mwenzake Mashali wa Tanzania wanatarajia kupambana katika Ukumbi wa Friends Corner ulioko Manzese jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pambano la kuwania Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati katika uzito wa kati (middle) kg 72.5.

Historia ya Sebyala kimchezo inaonesha amewahi kupambana na bondia Francis Cheka mjini Morogoro kuwania Ubingwa wa UBO, na pia kuzichapa na Rashid Matumla na kutoa upinzania mkali japo alimaliza mapambano hayo kwa kushindwa kwa pointi. Kwa upande wa mpinzania wake Mashali amekuwa akiwapa adhabu kali wapinzani wake kwa kuwatwanga kwa knock-out za mapema, isipokuwa kwa Seleman Galile aliyefanikiwa kunaliza pambano la kugombea TPBO uzito wa kati.

Aidha TPBO katika taarifa yake imesema mpambano wa mabondia hao pia ni mahususi kwa ajili ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. “Tumeamuwa kuwa kila tarehe ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere TPBO itakuwa inaandaa mapambano ya ngumi, ikiwa ni heshima kubwa kwa utawala wake wa Serikali ya Awamu ya Kwanza kutokana na jitihada za kusaidia michezo yote bila ubaguzi, kinyume na ilivyo sasa ambapo mchezo wa ngumi za aina zote umetupwa…,” ilisema taarifa ya TPBO kwa vyombo vya habari.