RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Mstaafu wa Zambia Kenneth Kaunda kuomboleza kifo cha mkewe, Mama Betty Kaunda, ambaye alifariki dunia Jumanne wiki hii akiwa na umri wa miaka 84.
“Nimesikitishwa na kushtushwa sana na taarifa za kifo cha Mama Betty Kaunda kilichotokea wiki hii mjini Harare, Zimbabwe, ambako alikuwa anamtembelea binti yake, Mama Musata Kaunda Banda. Mama Betty Kaunda alikuwa shujaa wa Bara letu na mama wa mfano siyo kwa wananchi wa Zambia bali kwa Waafrika sote. Kifo chake ni pigo siyo kwako tu Mheshimiwa Rais, ama kwa wanafamilia, ama hata kwa wananchi wa Zambia bali kwa Waafrika wote”.
Rais Kikwete amesema katika salamu zake hizo, “Kwa miaka yote alipokuwa mke wa Rais wa Zambia tokea Oktoba 1964 hadi Novemba 1991, Mama Betty Kaunda alikuwa nguzo ya familia na nguzo yako Rais katika mapambano ya kuleta uhuru wa Zambia na katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Mchango wake hautasahauliwa na pengo la kifo chake litabakia nasi kwa miaka mingi”.
“Mzee wangu Rais Kaunda nakutumia wewe salamu za dhati ya moyo wangu kufuatia kifo cha mama yetu na kupitia kwako kwa wanafamilia wote kwa kuondokewa na mhimili mkubwa wa familia.Naungana nanyi kuomboleza kifo cha mama yetu na pia naungana nanyi kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Betty Kaunda. Amen”.
Mama Kaunda ambaye ameacha watoto wanane, wajukuu 30 na vitukuu 11, alizaliwa Novemba 1928 katika Jimbo la Kaskazini mwa Zambia wakati huo ikiitwa Northern Rhodesia, akaolewa na Mzee Kaunda mwaka 1946 na karibuni walisherehekea miaka 66 ya ndoa yao mjini Lusaka, Zambia.