RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Meja Jenerali Samuel Albert Ndomba kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Meja Jenerali Ndomba kuwa Luteni Jenerali. Taarifa iliyotolewa, Septemba 21, 2012, mjini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu, imesema kuwa uteuzi huo unaanza mara moja.
Taarifa hiyo ya Balozi Sefue imesema kuwa kabla ya uteuzi wake, Meja Jenerali Ndomba alikuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Jenerali Ndomba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali Abdulrahman A. Shimbo ambaye amestaafu Jeshi kwa mujibu wa sheria baada ya kufikisha umri wa miaka 60.
Taarifa ya Balozi Sefue pia imesema kuwa Rais Kikwete amemteua Brigedia Jenerali Raphael Mugoya Muhuga kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa kuanzia leo, Ijumaa, Septemba 21, 2012.
Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Brigedia Jenerali Muhuga kuwa Meja Jenerali. Kabla ya uteuzi wake, Brigedia Jenerali Muhuga alikuwa Mkuu wa Utawala na Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).