Yanga Kushtakiwa Kwa Kuikashfu Hoteli Mbeya

Kocha Mkuu wa Timu ya Yanga, Tom Saintfiet

Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Chama cha Wamiliki wa Mahoteli Mkoa pamoja na mmiliki wa Peter Safari’s Hotel unatarajia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Timu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam kufuatia kauli ya kashfa iliyotolewa na Kocha Mkuu wa Timu ya Yanga, Tom Saintfiet.

Hivi karibuni Kocha Mkuu wa Yanga akizungumza na vyombo vya habari aliishutumu hoteli hiyo, akidai katika kipindi chote cha kufanya kazi Barani Afrika kwenye nchi takribani 20 hajawahi kulala kwenye hoteli yenye huduma mbovu kama aliyoikuta kwenye hoteli hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa na uongozi wa Hotel ya Peter Safaris umeitaka timu ya Yanga kujitokeza na kuomba radhi kabla uongozi wa hoteli hiyo ujachukua hatua za kisheria kutokana na lugha ambayo wamedai ni ya kuidhalilisha hoteli yao.

“Kimsingi management ya, tumesoma na kusikiliza na lawama zilizotolewa na Kocha huyo kuwa “hajawahi kulala kwenye hoteli ya hadhi ya chini kama hii katika nchi 20 alizowahi kufanya kazi katika nchi za Afrika,” imeeleza taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari.

“Uongozi wa hotel na chama cha wamiliki wa hotel kwa ujumla kinachukulia suala hili kama kampeni maalumu ya kudhalilisha na kukatisha tamaa wateja kuiona Mbeya haina hotel za hadhi za kuishi timu na watu wenye hadhi katika jamii, kitu ambacho si kweli na ni visingizio kutokana kushindwa kwake kuwezesha timu kufikia matarajio ya mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.”

“Kimsingi viongozi wa Timu ya Yanga waliomba kuwalaza wachezaji wawili katika kitanda kimoja tofauti na taratibu za hotel na hii ilitokana na mipangilio yao hasa kwenye suala la uwezo wa kulipia kila mchezaji chumba chake, aidha, uongozi wa hotel ulijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa wachezaji wanapata huduma walizohitaji na hata wakati mwingine kutoa usafiri kwa ajili ya kununua mahitaji ya familia zao kitu ambacho hakifanyiki maeneo mengine kwa gharama za hotel.”

“Kwa kutambua madhara yaliyotokana na matamshi ya kocha huyo raia wa Ubelgiji, Uongozi wa Hotel ya Peter Safaris unayaona matamshi haya kama udhalilishaji mkubwa na wenye nia mbaya ya kuuharibia Mkoa wa Mbeya na kuutangaza vibaya kwa wageni juu ya uwezo wake katika utoaji huduma za hoteli.”

“…Kwakuwa maneno ya kocha huyo yametamkwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari pasipo kukanushwa na viongozi wa Timu ya Yanga ambao ndiyo waliofanya maandalizi na kufanya mazungumzo ya maombi ya kuwalaza wachezaji wawili katika vyumba ambavyo vina uwezo wa kulaza mtu mmoja (single), Peter Safaris inaliona jambo hilo kama ni sehemu ya kashfa iliyojengwa kwa nia ya kuiharibia hotel biashara na kuipotezea hadhi mbele ya wageni na watumiaji wa huduma za Peter Safaris ambayo inaendelea kupanua huduma zake maeneo mengine.”

“Ikumbukwe kuwa Peter Safaris hotels imekuwa ikipokea wageni wa hadhi mbalimbali wakiwemo viongozi wa ngazi za kitaifa, wageni kutoka nje wa hadhi za juu na wafanyabiashara wakubwa, hivyo ugeni wa Yanga na hadhi inayozungumzwa na kocha huyo hauwezi kufikia mahala pa kuidhalilisha hoteli kwa kiwango hicho licha ya hotel kutopata maoni yoyote kwenye sanduku la maoni (suggestion box) baada ya timu kuondoka.”

“…Uongozi wa Hotel unautaka uongozi wa Yanga kuiomba radhi kwa lugha ya kashfa na isiyoendana na utamaduni wa Mtanzania kwa kuzingatia kuwa wachezaji wakiulizwa namna walivyohudumiwa wasingeweza kuzungumza hayo ambayo mwalimu wao ameyazungumza kwa utashi wake.

“Peter Safaris inalichukulia jambo hili kwa uzito unaostahili kwakuzingatia kuwa lugha iliyotolewa na mteja wake huyo imevuka kiwango cha kuvumilika, na njia pekee ambayo tunadhani ni ya uungwana kabla ya kuingia kwenye taratibu za kisheria ni kuwataka YANGA kuomba radhi kwa lugha ya dharau na kashfa dhidi ya hoteli,” imeeleza taarifa ya hoteli hiyo.
.