Kimisheni ya Ngumi Tanzania Yaisaidia BFT

Mchezo wa Ngumi Tanzania

Na Mwandishi Wetu

KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) imelipiga jeki Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Nchini (BFT) katika mashindano yaliyomalizika kwenye uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa kutoa zawadi za washindi kwanza na wa pili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Septemba 19, 2012 na Rais wa TPBC, Onesmo Ngowi imeeleza kamisheni hiyo ya ngumi imekabidhi kwa Katibu Mkuu wa BFT, Makoye Mashaga zawadi (fedha) za washindi wa kwanza na wa pili katika mashindano ya ngumi za ridhaa za taifa yaliyoshirikisha mabondia kutoka mikoa zaidi ya 19 ya Tanzania Bara.

Ngowi alisema kamisheni hiyo inaunga mkono juhudi za BFT katika kuendeleza ngumi nchini huku wakiamini kwamba katika mashindano kama hayo ndipo Tanzania inawapata wawakilishi wake katika mashindano ya kimataifa.

Ngowi alisema kuwa kama hakuna msingi mzuri wa ngumi za ridhaa ni wazi kuwa hakutakuwa na ngumi nzuri za kulipwa kwani msingi wa ngumi unaanzia kwenye ngumi za ridhaa.Rais huyo aliyekuwa bondia maarufu wakati wa ngumi za ridhaa na kulipwa miaka ya 80 na 90 kiasi cha lupewa jina la “Piston Mover”(mwendo wa piston ya gari) kwa ajili ya kasi ya mikono na miguu yake alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kufundisha ufundi kwa mabondia ili waweze kucheza ngumi za ufundi.

“Kuna tofauti kubwa sana kati ya ngumi za ridhaa na ngumi za kulipwa” aliendelea kusisitiza Rais huyo. Wakati mabondia wa ridhaa wanapewa points wakati wanapopiga ngumi za ufundi za kichwani, bondia wa ngumi za kulipwa anatakiwa aweze kumzidi mpinzania wake kwa kila kitu” aliendelea kusisitiza Rais huyo.

Mabondia wetu wa ridhaa wanatakiwa wafundishwe namna ya kupiga ngumi za ufundi kichwani na ziwe nyingi ndipo wanaweza kushinda kwenye mashindano ya kimataifa” alimalizia kusisitiza Ngowi.

Ushirikiano wa TPBC na BFT unaleta sura mpya kwenye tasnia ya ngumi nchini na inaonyesha mwanga mzuri mbele ta safari. Mgeni rasmi katika fainali za mashindano hayo alikuwa ni Katibu Mkuu wa BMT bwana Henry Lihaya na alimshukuru Ngowi kwa msaada huo wa TPBC. Hata hivyo, kiongozi huyo ndiye aliyekabidhi baadhi ya zawadi kwa washindi walioshinda katika fainali hizi za mwaka 2012.