Naibu Mkurugenzi Kufunga Mashindano ya Fainali za Ngumi Ubingwa wa Taifa

Mpambano wa ngumi

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Juliana Yassoda leo anatarajia kufunga Mashindano ya Fainali za Ngumi ya Ubingwa wa Taifa kwenye uwanja wa ndani wa taifa kuanzia saa tisa alasiri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Shirikisho la Mchezo wa Ngumi Tanzania (BFT), Makore Mashaga jana kwa vyombo vya habari katika fainali hizo mabingwa wa kila uzani wataibuka na medali za dhahabu pamoja na kitita cha sh. 30,000 kwa kila mmoja.

Kiongozi huyo wa BFT alisema michezo 9 ya mabondia wanaume na miwili ya mabondia wanawake itachezwa kwenye fainali hizo huku ikiwakutanisha mabondia wa uzani wa chini hadi ule wa juu, huku washindi wa pili kwa kila uzani wakiondoka na medali ya fedha na sh. 20,000 kila mmoja.

“Washindi wa tatu wa kila uzani watapata 10,000 kila mmoja pamoja na medali za Fedha,” alisema Mashaga na kuongeza kuwa kwa upande wa medali ya tatu washindi ni mabondia wawili katika kila uzani waliopoteza mapambano yao ya nusu fainali.

Katika mapambano ya jana, Said Hofu wa JKT alitinga fainali baada ya kumpiga Hafidh Bamtulah, wengine waliongia fainali ni Maulid Athuman Wa Polisi aliyempiga Maro James wa Ruvuma Mabondia wengine waliotinga fainali ni Mathar George wa Kilimanjaro atakayezichapa na Ireny Kimaro wa Tabora kwenye uzani wa light fly wakati Ester Kimbe wa Ngome atatoana jasho na Mariam Nyerere wa Dodoma katika uzani huo.

Aidha alisema matokeo ya wanaume ya nusu fainali iliyochezwa jana jioni kati ya Hashim Saimon wa Ngome na
Victor Njaiti wa JKT, Badi Mumbamba wa Temeke dhidi ya Seleman Bamtulah wa Magereza, Mohamed
Chibumbuli wa Magereza dhidi ya Omar Jongo wa Temeke alisema washindi waliopatikana ndio watakaocheza
fainali ya leo.
Mapambano mengine yalikuwa kati ya Alex Matero wa Temeke dhidi ya Joseph Martin wa JKT,
Yusuph Ndimbo wa Mbeya dhidi ya Shaban Ngaoneka wa Ilala, Yahaya Malik dhidi ya Hamad Furahisha.