Rais Kikwete Aweka Jiwe la Msingi Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi

Mfano wa Kituo Kikubwa cha Mabasi ya Mradi wa Usafiri wa Haraka Dar es Salaam (DART)

Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete leo, Septemba 19, 2012, ameweka jiwe la msingi kwenye Kituo Kikubwa cha Mabasi ya Mradi wa Usafiri wa Haraka Dar es Salaam (DART) katika sherehe iliyohudhuriwa na mamia ya wananchi katika eneo la Viwanja vya Jangwani katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya kuweka jiwe hilo la msingi katika sherehe ya kuvutia, Rais Kikwete ametembelea kwa muda mfupi na kukagua ujenzi wa Kituo cha Kimara ambako mtandao wa njia ya mabasi hayo utaanzia na kuingia katikati ya Mji wa Dar es Salaam.
Kwenye kituo hicho, Rais Kikwete amepewa maelezo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini, Injinia Patrick Mfugale kabla ya kwenda kwenye Viwanja vya Jangwani kuweka jiwe la msingi kwenye mradi mkubwa wa aina yake katika historia ya Tanzania na ambao lengo lake kuu ni kupunguza msongamano wa magari Dar es Salaam pamoja na kulipa Jiji hili usafiri wa kuaminika wa umma.
Mradi huo ambao utakuwa na mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 137, unajengwa kwa awamu sita na sherehe ya leo imeweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 20.9 na utakaohusisha barabara za Kimara-Kivukoni, Magomeni-Morocco na Fire-Kariakoo- Kivukoni.
Mradi huo utakuwa na njia maalum ya kupita mabasi yenye urefu wa kilomita 21, maegesho matatu ya mabasi (bus depots) mbili yaani moja Ubungo na nyingine Jangwani, vituo vikuu vitano ambavyo vitakuwa Kivukoni, Kariakoo, Morocco, Ubungo na Kimara, na vituo vidogo 29 ambavyo vitajengwa kila baada ya nusu kilomita.
Mradi huo unaogharimiwa na Benki ya Dunia kwa kiasi cha Sh. bilioni 240.879 ikiwa ni pamoja na fidia kwa mali za wananchi zitakazovunjwa katika kutekeleza mradi huo unajengwa na kampuni ya Strabag International ya Ujerumani na kusimamiwa na Kampuni ya SMEC International ya Australia. Hadi jiwe la msingi linawekwa leo, tayari Mradi huo umekwishajengwa kwa kiasi cha asilimia 20.
Injinia Mfugale amemwambia Rais Kikwete kuwa mtandao huo wa Mradi huo utakuwa na madaraja makubwa ya kuvukia wananchi matatu katika maeneo ya Kimara, Ubungo na Morocco.
Mradi huo ambao usanifu wake ulikamilika miaka mitano iliyopita unatarajiwa kukamilika na kufunguliwa rasmi mwanzoni mwa mwaka 2015 na inakadiriwa kuwa wamiliki wa kiasi cha daladala 1,800 zinazotoa huduma kwenye njia wa Mradi huo kwa sasa na ambazo zitakosa biashara baada ya kumalizika mradi, watapewa upendeleo maalum katika kununua hisa za Mradi huo.
Akizungumza Kimara na baadaye Jangwani, Rais Kikwete amesema kuwa Mradi huo ni sehemu ya juhudi kubwa za Serikali yake katika kuboresha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam na kuondoa msongamano wa magari kwenye mji huu.
“Juhudi zote hizi ni majawabu yetu kuhusu wingi wa magari katika Mji wetu. Ndio maana tunalenga kuanzisha usafiri wa watu wengi kama ilivyokuwa zamani hapa Dar Es Salaam,” amesema Rais Kikwete.
Ameongeza kuwa mipango mingine ya kupunguza msongamano ni pamoja na kujenga barabara za juu kwa juu (flyovers), kukabidhi baadhi ya barabara za Dar es Salaam kwa Tanroads na hata fikra ya kujenga barabara mbili kati ya Dar Es salaam na Chalinze, Mkoa wa Pwani.