NDOTO ya miaka mingi ya kujengwa kwa barabara ya Msata-Bagamoyo kwa kiwango cha lami imetimia Jumanne, Septemba 18, 2012, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara hiyo katika sherehe kubwa iliyofanyika eneo la Kiwangwa.
Barabara hiyo ya kilomita 64 inajengwa na mkandarasi wa ndani ya nchi, Estim Construction, na inagharimiwa asilimia mia na Serikali ya Tanzania bila msaada kutoka kwa mfadhili yoyote.Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania, Injinia Patrick L. Mfugale amesema kuwa barabara hiyo inayogharimu kiasi cha Sh. bilioni 94, ikiwa ni pamoja na fedha za fidia na kumlipa mkandarasi mshauri, itakamilika Juni mwakani.
Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais ameweka jiwe la msingi kwenye barabara hiyo, Injinia Mfugale amesema kuwa mkandarasi wa sasa alianza ujenzi tokea 2010 baada ya usanifu wa barabara hiyo kukamilika na baada ya Serikali kumtimua mkandarasi wa mwanzo wa barabara hiyo, TACOPA, Novemba 13, mwaka 2009.Amesema kuwa mpaka sasa barabara hiyo imekamilika kwa asilimia 65, yaani kwamba kiasi cha kilomita 36.7 tayari zimewekwa lami na kuwa ni kilomita 23 zilizosalia na ambazo zitamalizika katika miezi tisa ijayo.Injinia Mfugale amesema kuwa mpaka sasa Serikali imekwishakulipa kiasi cha Sh. bilioni 56.8 ikiwa ni pamoja na fedha iliyolipwa kama fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo hautahusisha ujenzi wa daraja kwenye Mto Ruvu kwa sababu usanifu wa daraja hilo ulichelewa kidogo kukamilika hata kama tayari sasa umekamilishwa.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John P. Magufuli amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya ujenzi wa kilomita 11,154 za barabara za lami zinazojengwa na Serikali ya Mheshimiwa Kikwete.“Nataka muelewe vizuri maana ya kilomita hizi. Wakati wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, tulikuwa na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,330. Kati ya Uhuru na mwaka 2005, tulijenga barabara zenye urefu wa kilomita 6,500 na kati ya 2005 na sasa tunajenga barabara zenye urefu wa kilomita 11,154,” amesema Waziri Magufuli.Waziri huyo amerudia msimamo wake kuwa kamwe Serikali haitawaachia watu wanaojenga ama kufanya shughuli katika eneo la hifadhi ya barabara bila kuwachukulia hatua.
Naye Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi walioshiriki katika sherehe hizo kuwa barabara ndiyo mishipa ya damu ya uchumi wa nchi yoyote na ndiyo maana Serikali inatenga kiasi kikubwa katika Bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Amesema kuwa katika Bajeti ya sasa, barabara zimetengewa kiasi cha Sh. trilioni 2.2 ambacho ni kiasi kikubwa cha pili baada ya Bajeti ya elimu.Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na faida zake kubwa na nyingi, barabara hiyo itakuwa na changamoto zake ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ajali za barabara, kuongeza urahisi wa kusambaa kwa ugonjwa wa ukimwi na hata kuvutia watu wenye lengo la kununua ardhi kubwa ya wanavijiji ambako inapita barabara hiyo.Rais pia ameungana na Waziri Magufuli kwa kuonya: “Kama alivyosema Waziri, wanaoifuata barabara watavunjiwa nyumba zao na hawatalipwa, lakini wale ambao barabara inawafuata watalipwa hata wakivunjiwa.”