MBUNGE wa Afrika Mashariki Shy-Rose amekichangia Chama Cha Wanahabari Wanawake nchini –TAMWA jumla ya shilingi milioni mbili.
Akiukabidhi mchango huo katika ofisi za TAMWA jijini Dar es salaam, Shy-rose amesema TAMWA inastahili pongezi na kuungwa mkono kutokana na kazi kubwa inayofanywa kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
“Kikubwa zaidi nimeona TAMWA imekuwa na sauti kubwa kutetea wanawake hasa wajane na watoto,” alisema Mbunge huyo wa Afrika Mashariki ambaye pia ni mwanahabari mahiri anayejituma kwa dhati kutumikia wananchi.
Ameiomba jamii, mashirika na watu wenye mapenzi mema kutambua mchango wa TAMWA hasa katika kutetea haki za wanawake na watoto na kuunga mkono harakati hizo kwa hali na mali.
“Bila uwepo wa TAMWA tusingekuwa tumefikia hatua hii tuliyofikia kama taifa”, alisema Bhanji.
Sisi TAMWA tunamshukuru kwa dhati Shy-rose Bhanji kwa mchango wake kwa TAMWA tunamwahidi yeye binafsi na taifa letu kwa ujumla kwamba mchango wake kama ilivyo michango mingine utatumika kikamilifu kuimarisha shughuli tunazozifanya za utetezi wa haki za wanawake na watoto.
Tangu TAMWA ilipoanzishwa mwaka 1987, imekuwa ikitumia vyombo vya habari kwa ajili ya kuelimisha na kuhamasisha jamii kuchukua hatua kuondoa mila, desturi na sheria zinazowanyima haki wanawake na watoto.