Na Mwandishi Maalum
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi kufuatia taarifa za ajali ya barabarani iliyohusisha lori aina ya Isuzu lililopinduka huku likiwa limebeba abiria katika eneo la Relya katika Kijiji cha Bereko, Wilaya ya Kondoa katika Mkoa wa Dodoma siku ya Jumamosi tarehe 15 Septemba, 2012 ambapo watu 15 walipoteza maisha papo hapo na wengine 72 kujeruhiwa.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa na ajali hii ya lori ambayo, katika kipindi kifupi tangu itokee ajali nyingine iliyogharimu maisha ya watu wengi katika Mkoa wa Mara, imeondoa tena uhai wa watu wetu wengine 14 wasiokuwa na hatia”, amesema Rais Kikwete kwa masikitiko na kuongeza
“Mamlaka zote zinazohusika hazina budi kuunganisha nguvu katika kukabiliana na wimbi la ajali za barabarani za mara kwa mara zinazokatisha uhai wa watu wengi wasiokuwa na hatia ambao kimsingi ni nguvu kazi muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu”.
“Kufuatia ajali hiyo, ninakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi Salamu za Rambirambi kwa kuwapoteza watu wengi katika Mkoa wako. Kupitia kwako naomba Salamu za Rambirambi na pole nyingi ziwafikie wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao. Namuomba Mwenye Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu mahala pema peponi, Amina”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Vilevile Rais Kikwete amesema anawaombea kwa Mola wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ili waweze kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida na kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao. Aidha amesema anawaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza vifo vya wapendwa wao.