RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tupa kufuatia vifo vya watu 13, na wengine 13 kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace walilokuwa wakisafiria kupasuka tairi la nyuma na kusababisha kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea Septemba 11, 2012 katika eneo la Mkiringo kwenye Barabara ya Mwanza – Musoma katika Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara, wakati basi hilo likiwa linasafirisha abiria kutoka Musoma mjini kwenda Nyamusu kupitia Butiama.
Katika Salamu zake za Rambirambi, Rais Kikwete amesema anasikitishwa na kuhuzunishwa anapoona maisha ya watu yakiendelea kupotea kutokana na ajali za barabarani ambazo zinaweza kuzuilika endapo Sheria ya Usalama Barabarani itasimamiwa kikamilifu na Mamlaka husika, na madereva kuiheshimu na kuizingatia kikamilifu Sheria hiyo wanapoendesha magari yao.
“Ninasikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za mara kwa mara za ajali za barabarani ambazo zinagharimu maisha ya watu wengi wasiokuwa na hatia kwa sababu ya kutozingatiwa na kusimamiwa kikamilifu kwa Sheria ya Usalama Barabarani. Ni vema vyombo vinavyohusika vikaimarisha zaidi usimamizi wa Sheria hii ili maisha ya Watanzania yasiendelee kupotea”, amesema Rais Kikwete.
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa John Gabriel Tupa, Salamu za Rambirambi, na kupitia kwako naomba Salamu hizi ziwafikie pia wanafamilia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hiyo”.
“Namuomba Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema azilaze mahala pema peponi Roho za Marehemu, na awape moyo wa uvumilivu na subira wote waliofikwa na msiba huo,” ameongeza kusema Rais Kikwete.
Vilevile Rais Kikwete amesema anamuomba Mola awawezeshe kupona haraka majeruhi wote wa ajali hiyo, ili waweze kurudi katika hali yao ya kawaida na kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao.