SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litatoa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 7.3 kwa Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam ambazo ni asilimia 5 ya fedha zilizopatikana kwenye mechi ya Simba na Azam.
Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa 2012/2013 ilichezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuingiza sh. 146, 640,000. Washabiki 26,001 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda mabao 3-2. Sekretarieti ya TFF inatarajia kukutana na uongozi wa Hospitali ya Temeke wakati wowote kuanzia leo ili kujua mahitaji halisi kabla ya kufanya ununuzi wa vifaa husika.
Mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo uliokuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 22,368,813.56, asilimia 5 ya mchango wa kusaidia jamii (Hospitali ya Temeke) sh. 7,332,000, uwanja sh. 10,148,318.64, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,059,327.46, TFF sh. 10,148,318.46 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,074,159.32.
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 1,014,831.86, kila timu sh. 32,265,025.93, asilimia 10 ya gharama za mchezo sh. 10,148,318.64, nauli kwa waamuzi na kamishna sh. 80,000, posho ya kujikimu kwa waamuzi na kamishna 230,000, posho ya waamuzi 400,000, tiketi sh. 4,495,800, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi uwanjani sh. 2.350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000.000.
Mchango wa kusaidia jamii kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu uliopita kati ya Yanga na Simba ulikuwa sh. 15,000,000 ambazo zilikwenda Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kusaidia uchunguzi wa kansa ya matiti kwa akina mama.
Wakati huo huo, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Septemba 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam imepitisha marekebisho ya kanuni kwa ajili ya Ligi ya Mkoa na Ligi ya Wilaya. Marekebisho hayo yametokana na mabadiliko ya mfumo wa mashindano uliofuta Ligi ya Taifa. Hivi sasa kutakuwa na Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Mkoa na Ligi ya Wilaya.
Kutokana na marekebisho hayo ya kanuni; Ligi ya Wilaya itaendeshwa na Vyama vya Mpira wa Miguu vya Wilaya (DFAs), Ligi ya Mkoa itaendeshwa na Vyama vya Mpira wa Miguu vya Mikoa (RFAs).
Mechi za mchujo (play offs) kutafuta timu zitakazopanda kwenda Ligi ya Mkoa zitaendeshwa na RFAs wakati play offs za kupanda Ligi Daraja la Kwanza zitakazohusisha mabingwa wa mikoa zitasimamiwa na TFF. Ligi za madaraja yote zitachezwa mwaka mzima kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.