Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewasili nchini Kenya Septemba 11, 2012, kuanza Ziara Rasmi ya Kiserikali (State Visit) ya siku tatu ikiwa ni ziara yake ya kwanza rasmi nchini humo ingawa amefanya ziara kadhaa za kikazi nchini Kenya.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, Rais Kikwete ambaye amefuatana na mkewe, Mama Salma Kikwete, amepokewa na mwenyeji wake, Rais Mwai E. Kibaki na kwa mbwembwe zote za kiprotokali zinazoambatana na ziara rasmi za kiserikali.
Baadaye mchana, Rais amekwenda Ikulu ya Kenya ambako ametia saini kitabu cha wageni, akafanya mazungumzo ya faragha na Rais Mwai Kibaki kabla ya kufanyika kwa Mazungumzo Rasmi ya Kiserikali kati ya nchi hizo mbili majirani na wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete na ujumbe wake amekwenda kwenye Chuo Kikuu cha Kenyatta ambako umepokewa na Waziri wa Elimu ya Juu, Margaret Kamar, Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstaafu Onesmus Mutungi na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Olive Mugendi.
Kwenye chuo hicho ambacho Desemba 8, mwaka 2008, kilimtunuku Rais Kikwete Shahada ya Uzamivu ya Heshima, amefungua rasmi Jengo la Shule ya Ukarimu na Utalii ya Chuo hicho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Shule hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa utalii ni sekta muhimu sana katika chumi za nchi za Afrika Mashariki na ambayo mchango wake unagusa maisha ya maelfu kwa maelfu ya wananchi wa nchi za ukanda huo.
Rais pia amesema kuwa nchi hizo za Afrika Mashariki sasa zimekuwa ni eneo lenye mvuto mkubwa katika nyanja ya utalii ambao unaweza kuwaingizia wananchi na mataifa ya Afrika Mashariki mapato zaidi kama changamoto zinazoikabili sekta ya utalii kwa sasa zitashughulikiwa ipasavyo na kwa pamoja na nchi hizo.
Miongoni mwa changamoto ambazo Rais Kikwete amezitaja ni ukosefu wa miundombinu ya kutosha kufanikisha kwa namna bora zaidi sekta ya utalii, ukosefu wa juhudi za pamoja kuitangaza Afrika Mashariki kama eneo muhimu la utalii, na umuhimu wa kuboresha kiwango cha usalama wa watalii.
Aidha, Rais Kikwete amezielezea changamoto nyingine kuwa ni pamoja na umuhimu wa kuwepo na viza ya pamoja ya utalii kwa nchi zote za Afrika Mashariki, kuwepo kwa safari za ndege za kutosha kutoka kwenye mataifa makubwa yanayozalisha watalii kwa wingi kuja Afrika Mashariki na umuhimu wa kupungua kwa nauli za ndege za kuja Afrika Mashariki.
Leo jioni, Rais Kikwete anatembelea Taasisi ya Utatifi wa Kilimo ya Kenya (KARI) ambako anatarajiwa kupokelewa na Waziri wa Kilimo wa Kenya, Mheshimiwa Dr. Sally J. Kosgei na usiku atakuwa mgeni rasmi kwenye Dhifa ya Kitaifa ambayo itaandaliwa na mwenyeji wake, Rais Mwai Kibaki.
Kesho, Rais Kikwete ataweka shada la maua kwenye Kaburi la Mwanzilishi wa Taifa la Kenya, Hayati Jomo Kenyatta, kwenye Viwanja vya Bunge la Kenya na kutembelea Kiwanda cha Maziwa cha Brookside Diary kwenye Barabara ya Thika.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara yake, Rais Kikwete atatembelea Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya (National Defence College) kilichoko Karen, Nairobi, ambako atapokelewa na Waziri wa Nchi wa Ulinzi, Yusuf Haji na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Julius Karangi.
Baadaye, Rais Kikwete atakwenda kutembelea Kituo cha Magonjwa ya Moyo na Kansa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan ambako atapokelewa na Waziri wa Huduma za Matibabu, Anyang Nyong’o.
Baadaye jioni, Rais Kikwete ambaye anaongozana na kundi kubwa la Wafanya Biashara wa Tanzania atashiriki chakula cha jioni ambacho ameandaliwa na Jumuiya ya Wafanya Biashara ya Kenya.