Polisi Kilimanjaro Wageuza Madawa ya Kulevya ‘Dili’

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz

Na Mwandishi Wetu, Moshi

SERIKALI mkoani Kilimanjaro imekiri madawa ya kulevya ni tatizo katika mkoani huo na wapo baadhi ya askari polisi wamegeuza madawa hayo kuwa biashara jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Manispaa ya Moshi mkoani humo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Bondeni ambapo wananchi walilalamika kuzagaa kwa madawa ya kulevya mtaani hali ambayo imeonekana kuwaathiri vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Gama alisema tatizo la madawa ya kulevya si la kata ya bondeni wala manispaa ya Moshi pekee bali ni tatizo la mkoa mzima wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla ambalo linapaswa kushughulikiwa na kuhakikisha linakomeshwa ili kuweza kulinusuru taifa.

Gama alisema kumekuwepo na taarifa za baadhi ya askari polisi katika mkoa wa Kilimanjaro, ambao wamegeuza madawa ya kulevya kuwa biashara, jambo ambalo ni hatari na linafifisha jitihada za Seriikali za kupiga vita madawa ya kulevya nchini. Alisema zipo taarifa pia kuwa wapo askari ambao hupita manyumbani kwa watu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya na kuokota fedha, ili kuficha uovu wao, ili hali wakijua kabisa kuwa ni kosa kisheria.

Alisema askari polisi kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ni tatizo kubwa, ambalo linapaswa kushughulikiwa mara moja na kwa atakayebainika kuchukuliwa hatua kali za kisheria, ili kuweza kulikomesha tatizo hilo.

“Madawa ya Kulevya ni tatizo kubwa kwa sasa, kwani mengine yanapita mipakani kwetu, manyumbani mwetu na mmesikia pia katika uwanya wetu wa ndege wa Kimataifa KIA yamekamatwa madawa ya kulevya, hii ni hatari sana kwani vijana ndio wamejiingiza katika biashara hii na wengine kwa sasa hawawezi kufanya tena kazi kwa sababu ya kuathiriwa na madawa haya, kwakweli tusipolidhibiti hili kwa nguvu zetu zote, tunalea taifa ambao halifai chochote,” alisema Gama.

Kufuatia hali hiyo mkuu huyo wa mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Ibrahim Msengi na Mkuu wa Kituo cha Polisi Moshi kufuatilia suala hilo kwa haraka ili kulidhibiti na kuwabaini askari ambao wanajihusisha katika biashara hiyo.

Aidha mkuu huyo pia aliwataka wananchi mkoani humo, kutoa ushirikiano katika kupambana na madawa ya kulevya na kuwataja wafanyabiashara wa madawa hayo pamoja na askari ambao wamekuwa wakihusika.

Awali wakizungumza wananchi walisema madawa ya kulevya kwa sasa yamekuwa tishio katika manispaa hiyo hususani eneo la kata ya Bondeni, na kwamba magari madogo ya abiria yanayofanya safari zake maeneo mbalimbali katika manispaa hiyo ambayo huegeshwa eneo la manyema ndiyo yamekuwa yakitumika kusambaza madawa hayo.