Na Mwandishi Wetu, Moshi
WANANCHI wa Kata ya Bondeni Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia ukosefu wa choo katika kata hiyo ambayo ina soko limalotumiwa na wafanyabiashara mbalimbali ikiwemo wa samaki wabichi hali ambayo inahatarisha maisha yao kwa sasa.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jana eneo la manyema katikakata hiyo wananchi hao walisema ukosefu wa choo katika eneo hilo umekuwa ni tatizo kubwa ambalo limesababisha maeneo mbalimbali ya kata hiyo ikiwemo eneo la reli kugeuzwa choo na wafanyabiashara.
Walisema ni hatari sana kukosekana kwa choo katika eneo la soko mbapo hukutana watu wengi na huuzwa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula hivyo ni vema Serikali ikaliangalia hilo kwa haraka ili kuweza kuwanusuru wananchi na magonjwa ya milipuko. Walisema katika soko hilo wafanyabiashara wamekuwa wakitozwa ushuru lakini cha kushangaza ni kwamba hakuna choo hali ambayo inahatarisha maisha ya wafanyabiashara na wanunuzi.
“Katika eneo hili la bondeni panauzwa samaki wabichi na biashara nyingine, lakini hakuna choo, hii imesababisha wafanyabiashara na wananchi wengine wanaokuja katikaoko hili kugeuza eneo la reli kuwa choo na wengine kutumia maeneo ya pembeni mwa soko hili ambapo huegeshwa magari na kwenye nyumba za watu na hii imesababisha vinyesi kutapakaa kila eneo, hii ni hatari sana, tunaomba tatizo hili lishughulikiwe,” alisema Ally Mrisho.
Aidha wananchi hao walisema pamoja na uchafu wa vinyesi pia kumekuwepo na tatizo lingine la uchafunzi wa mazingira ikiwemo wa matairi ya magari na taka nyingine ambapo katika eneo hilo, kumekuwa kama dampo. Walisema pamoja na Mji wa Moshi kusifika kwa usafi nchi nzima bado katika eneo lao kumekuwa kukizagaa aina mbalimbali za uchafu ili hali manispaa hiyo imeweka wasimamizi wa usafi.
Akijibu malalamiko hayo Mkurugenzi wa manispaa ya Moshi Bernadette Kinabo alisema suala la uchafu katika kata ya Bondeni ni changamoto kubwa inayoikabili manispaa hiyo na kwamba wamejipanga kulishughulikia na kuhakikisha wanalimaliza.
“Kutapakaa kwa vinyesi mitaani na kwenye nyumba za watu na uchafuzi wa mazingira, ni kero kubwa na linatukera sana hata sisi manispaa, kwani manispaa tunazalisha taka zaidi ya tani 250 kwa siku, tutalishighulikia hili ili kuhakikisha tunalimaliza,” alisema Kinabo.
Aidha aliwataka wananchi kukubali kulipa ushuru wa sh. 200 kwa ajili ya matumizi ya choo ili kuweza kupata huduma safi na sahihi na kuepusha tatizo la kutapakaa kwa vinyesi mitaani kutokana na kwamba, kumekuwepo na choo katika soko la mbuyuni linalopakana na eneo linalouza samaki lakini wananchi wamegoma kulipia kodi ya choo hivyo kugeuza maeneo mbalimbali kuwa choo.