Utata waibuka maandamano ya waandishi wa habari

Waandishi wa Habari katika Maandamano yao


Na Bashir Nkoromo


MAANDAMANO
ya Waandishi wa habari kulaani mauaji ya Mwandishi wa habari, Daud Mwangosi yameingia utata baada ya waandishi kumfukuza Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi lakini wakamkaribisha kada wa CHADEMA kuwahutubia. Utata huo ulijitokeza kwenye viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, baada ya waandamaniji kufika wakiwa na viongozi wao wakiwemo kutoka Jukwaa la Wahariri.

Mara msafara huo ulipofika, pembezoni mwa viwanja hivyo, ukakumbana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchini alikiwa eneo hilo na mara akaungana na baadhi ya viongozi wa waandishi, ambao walijaribu kutaka kumtamtambulisha.

“Hatuatakiii, aondoke, aondoke!” waandishi wa habari kwenye maandamano hayo walipaza sauti huku wengine wakirusha mikono kuashiria kukataa kabisa waziri Nchini asizungumze lolote au kuwepo kwenye mkutano mwishoni mwa maandamano hayo.

Baadhi ya viongozi wa Jukwaa la Wahariri akiwemo Nevilli Meena, walijaribu kuwatuliza waandishi lakini, ikashindikana na kwa busara Waziri Nchini akaamua kuondoka. Hata hivyo katika kinachoonesha kwamba kulikuwepo tofauti kati ya waandishi kuhusu kumkataa Dk. Nchini, baadhi yao walimfuata na kumhoji, lakini wengine wakaingilia kati kuzuia mahojiano hayo.

“Sasa tumesema aondoke halafu mnamhoji, mnamhoji nini na tumekataa hapa asiseme nini? mwacheni njooni kwenye mkutano wetu hapa, kwanza sijui habari hizo mtazirusha wapi, sisi ndiyo wahariri”, zilisikika sauti zikipazwa.

Baada ya kuzungumza viongozi mmoja baada ya mwingine, wote wakilaani kwa nguvu zote mauaji ya Mwangosi, nayoaminika kufanywa na polisi wakati wa maandamano ya Chadema, Septemba 2, mwaka huu, mkoani Iringa, ndipo akapandishwa jukwaani Kada wa Chadema, Dk. Azaveri Rweitama. Dk. Rweitama ambaye amewahi kushiriki shughuli nyingi za Chadema ikiwemo mikutano ya chama hicho, alipandishwa jukwaani mmoja wa viongozi wa Jukwaa la Wahariri.

“Jamani mnajua waandishi wa habari tuna marafiki. Sasa hapa tunaye Dk. Rweitama amabaye ni rafiki yetu atazungumza machache”, alisema Misango akimkaribisha Dk. Rweitama.

Akizungumza, Reitama aliwataka waandishi wa habari kutowachukia polisi wadogo akisema, wao siyo tatizo ila tatizo ni wakubwa zao ambao alidai wanatumwa na wanasiasa kutekeleza matakwa yao.

“Sasa kama Chadema wanafungua matawi ya chama chao, kwa nini utumie polisi kuwazuia? si na wewe ukafungue matawi yako?” alisema Dk. Reitama katika moja hoja zake kwenye mkutano huo.

Kufuatia Dk. Reitama kuzungumza habari za vyama vya siasa hadi kutaja majina, baadhi ya viongozi na waandishi walianza kulauminiana kuonyesha kwamba walichofanya nin kosa.

“Sisi tulikuwa tumeshakubaliana kwamba asishirikishwe kada wa chama chochote wala wanaharakati, sasa huyu Rweitama nani amemruhusu kupanda jukwaani?, alihoji mmoja wa viongozi wa Klabu wa Waandishi wa habari wa Dar es Salaam.

Maandamano ya waandishi hao yalianzia kituo cha Channel Ten, jijini, saa tatu asubuhi, na kuendelea hadi kwenye viwanja hivyo vya Jangwani, baada ya kupitia barabara ya Morogoro. Polisi walisindikiza maandamano hayo baadhi wakiwa nyuma na gari lao na wengine wakitembea kwa miguu, hadi kwenye viwanja hivyo, ambako halimalizika salama.

– nkoromo@gmail.com