*Wamtimua kwenye maandamano alipotaka kuyapokea
Na Joachim Mushi
MAANDAMANO ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam yamegeuka uchungu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi baada ya wanahabari hao waliokuwa katika maandamano kumtimua waziri kwenye viwanja vya Jangwani alipofika kwa nia ya kupokea maandamano hayo.
Waziri Dk. Nchimbi amekubwa na kadhia hiyo leo baada ya kuwasili katika viwanja vya Jangwani tayari kwa kuyapokea maandamano ya wanahabari walioandamana kimya kimya majira ya saa tatu asubuhi wakitokea zilipo ofisi za Kituo cha Channel 10 kwenda viwanja vya Jangwani.
Wanahabari hao ambao walikuwa na mabango mbalimbali yaliokuwa yamebeba jumbe za kuonesha kukerwa dhidi ya mauaji yaliotokea hivi karibuni ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel 10 mkoani Iringa, Daud Mwangosi, walipowasili katika viwanja vya Jangwani walimkuta Waziri Nchini akiwa eneo hilo kwa nia ya kupokea maandamano hayo; lakini ziliibuka kelele za wengi wao wakimtaka aondoke eneo hilo kwani hawamuhitaji.
“Tunaomba Waziri Nchimbi aondoke wala hatumtaki kwani yeye ni miongoni mwa watu (Serikali) ambao
tunawalalamikia dhidi ya mauaji yaliotokea. Kama mnataka usalama tunaomba ashuke jukwaani na aondoke hatumuitaji,” zilisikika kelele za baadhi ya wanahabari zikisema.
Aidha baada ya mayowe hayo viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambao ni waratibu wa maandamano hayo walizungumza na Waziri Nchini na baadaye aliteremka jukwaani na kuelekea kwenye gari lake na kuondoka eneo la Jangwani.
Katika viwanjwa hivyo viongozi mbalimbali wa vyombo vya habari (Wahariri) walitoa matamko wakionesha kukerwa na tukio zima lililosababisha kifo cha Mwangosi huku wakilaani Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuwathamini waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao na kuwaona ni maadui kwao.
Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamuhuri, Manyerere Jakton alisema kitendo cha kuuwawa kwa mwanahabari Mwangosi tukio ambalo ni la kikatili kutokea kwa wanahabari ni juhudi za kuzima uhuru wa vyombo vya habari nchini, jambo ambalo alisema halipaswi kufumbiwa macho hata kidogo.
Aidha mhariri huyo mkongwe nchini alisema tukio la kuuwawa kwa Mwangosi Jeshi la Polisi halina budi kulichukulia tukio hilo kama mwanzo wa kurekebisha utendaji mbovu kwa wanahabari pindi wanapokuwa katika majukumu yao. “Damu ya Mwangosi uwe mwanzo wa polisi kurekebisha utaratibu wao kiutendaji,” alisema Jakton.
Mhariri Mkuu wa Gazeti la Nipashe, Jesse Kwayu akizungumza alisema Jeshi la Polisi alina budi kuwa makini katika utendaji wao wa kazi kwani wanapaswa kuwalinda kikamilifu raia ukizingatia kuwa wao ndiyo walipakodi ambayo hutumika kuwalipa mishahara askari kwa majukumu yao.
Alilitaka Jeshi la Polisi kutambua majukumu ya waandishi wa habari na kutowaingilia wakati wakitimiza wajibu wao jambo ambalo limekuwa la kawaida hivi sasa baadhi ya wanahabari kuzuiwa na hata kudhuriwa ama kunyanyaswa wakati wakitekeleza majukumu wao. Aliitaka Serikali kuhakikisha inasimamia haki juu ya suala zima ili waliohusika na kifo cha Mwangosi waandibiwe kwamujibu wa sheria za nchini.
Naye Katibu Mkuu wa TEF, Nevilli Meena akizungumza katika maandamano hayo alisema wameamua kuandamana ili kuweka kumbukumbu ya kulaani tukio lililotokea na kuutaka umma utambue kuwa kwa sasa mazingira ya utendaji kazi kwa wanahabari si salama tena hivyo kuvitaka vyombo husika viliangalie suala hilo kwa makini.
“Jeshi la Polisi jana lilitaka kuzuia maandamano yetu, lakini tunataka watambue kuwa tunamadaraka makubwa na hata tungeliweza kutumia vyombo vyetu vya habari kufanya kitu cha zaidi ya maandamano…tukiamua kutumia vyombo vya habari na kulipiza kisasi dhidi ya Polisi hali ingelikuwa mbaya zaidi, hatukutaka kufanya hivyo,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa wanasubiri ripoti ya Serikali juu ya tukio zima na ile ya kihabari ambayo TEF imeunda timu kisha baada ya hapo watatoa msimamo wa wanahabari kuhusiana na suala hilo. Mmoja wa wajumbe ya Bodi ya TEF, Masoud Sanani akizungumza alisema kwa sasa ndani ya siku 40 za maombolezo ya kifo cha Mwangosi wanahabari wamesusia kuandika habari za polisi.
Katika mkusanyiko huo wanahabari walichanga jumla ya sh. 526,000 fedha ambazo zilikabidhiwa kwa uongozi wa kituo cha Channel 10 kama rambirambi ya kifo cha Mwangosi ambazo zitakabidhiwa kwa familia ya mwanahabari huyo.