MAKAMU wa rais wa Iraq Tareq al-Hashemi amepinga hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi yake na mahakama nchini humo jana kwa makosa ya kuhusika na kupanga mauaji na kujigamba kwamba hukumu hiyo ni kama medali kifuani mwake.
Makamu huyo wa rais ambaye ni moja wa waumini wa madhehebu ya sunni wenye vyeo vya juu kabisaa katika serikali ya Iraq amewaambia waandishi wa habari mjini Ankara, Uturuki kuwa anaipinga hukumu hiyo kwa vile kesi iliyofunguliwa dhidi yake ilichochewa kisiasa, na kumshtumu waziri mkuu Nouri al-Maliki kwa ukandamizaji dhidi ya waumini wa madhehebu ya sunni.
Waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki ambaye Hashemi anamshtumu kwa kumuandama kisiasa.
“Nakataa kabisaa, na kamwe sintotambua hukumu hiyo isiyo ya haki na yenye malengo ya kisiasa, ambayo ilitarajiwa tangu mwanzo wa kesi hii ya kuchekesha. Naichukulia hukumu hii kama medali kifuani mwangu, na gharama ya haki ambayo napaswa kulipwa kwa utumishi wangu uliyotukuka kwa nchi yangu Iraq na kwa wantu wangu, raia wa Iraq,” alisema hashemi.
Hatari ya kuongezeka kwa vurugu za kidini
Wachambuzi wanasema hukumu hii inaweza kuchochea zaidi vurugu za kidini, baada ya siku mbaya ya mauaji ambapo watu wasiyopungua 88 waliuawa katika matukio mfululizo ya uripuaji wa mabomu. Hashemi aliikimbia Iraq baada ya mamlaka kutoa waranti wa kukamatwa kwake mwezi Desemba katika hatua ambayo ilitishia kuvunja makubaliano ya kugawana madaraka kati ya washia, wasunni na Wakurdi wakati ambapo majeshi ya Marekani yalikuwa yakiondoka nchini humo.