Wapiga kura mil 2.6 walikuwa feki Zimbabwe

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe

ORODHA ya wapiga kura iliyofichuliwa katika daftari la kudumu la wapiga kura nchini Zimbabwe hivi karibuni imebaini kuwa majina ya wapiga kura hewa ni milioni 2.6, wapiga kura hawa feki waliingizwa ili kuendeleza udanganyifu.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika moja linaloheshimiwa sana nchini Afrika Kusini ‘South African Institute of Race Relations’ lililofanya utafiti juu shughuli zima la kuandikisha wapiga kura.

Orodha hiyo inaashiria kuwa kuna zaidi ya watu 41,000 walio na umri wa zaidi ya miaka 100, hii ikiwa ni mara nne zaidi ya idadi ya watu hao nchini Uingereza, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya watu na muda mrefu wa kuishi ikilinganishwa na Zimbabwe.

Tofauti hiyo ya kura inatosha kuamua matokeo ya uchaguzi wowote utaoandaliwa Zimbabwe. Rais Robert Mugabe tayari ameitisha uchaguzi ufanyike mwaka huu, licha ya mpinzani wake wa siku nyingi, na Waziri Mkuu katika Serikali ya Mseto, Morgan Tsvangirai, kupinga akitaka uchaguzi huo kuandaliwa mwaka 2012 baada ya katiba mpya kuidhinishwa ili kuhakikisha kuna uhuru na haki.

Uchaguzi wa mwaka 2008 nchini humo ulikumbwa na vurugu dhidi ya wafuasi wa Tsvangirai, na wachambuzi wamedai kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa katika kura za awali. Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kati ya wafuasi wa Mugabe na Tsvangirai katika siku za hivi karibuni huku uchaguzi huo ukikaribia.

Utafiti ulibaini kuwa ingawa Zimbabwe umri wa kuishi miongoni mwa raia wa Zimbabwe imeteremka hadi miaka 49, kulikuwa na wapiga kura 41,100 wanaodaiwa kuwa na zaidi ya umri wa miaka 100, huku watu 16,800 walikuwa na siku moja ya kuzaliwa (Januari Mosi 1901). Majina ya watu waliofariki hayajaondolewa kwenye orodha hiyo, ilhali wapiga 230 walionekana ni wana umri wa chini ya miaka 18.