RC Kilimanjaro atoa somo kwa wahandisi

Moja ya majengo yanayojengwa na wahandisi wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Moshi

WAHANDISI wa ujenzi mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kujenga majengo kwa tahadhari kulinaga na mazingira ya eneo husika, hatua ambayo itasaidia kuepuka maafa ikiwemo ya moto ambayo hutokea na kusababisha madhara makubwa na hata vifo kutokana na wahusika kukosa pa kupita ili kuweza kujiokoa.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama, mara baada ya kutembelea Bweni la wasichana la kidato cha tano katika shule ya sekondari muungano iliyopo wilaya ya Moshi mkoani humo na kukuta bweni hilo limezibwa juu kote na kuwekwa milango ya chuma hali ambayo alisema ni hatari sana kwa wanafunzi.

Bw. Gama alisema majengo mengi ya serikali hasa ya shule yamekuwa hayajuengwi kwa tahadhari, hali ambayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa hasa pale ambapo moto hutokea jambo ambalo alisema kwa sasa linapaswa kuepukwa kwa kujengwa majengo kwa tahadhari.

“Jengo ni nzuri ila sijaridhika na ramani yake,mmeliziba kabisa, hii ni hatari sana kwani hata kukitokea moto huko ndani wanafunzi hawana pa kukimbilia watateketea wote, hii ni hatari sana,wahandisi kuweni makini katika hili”alisema Bw. Gama.

Aidha Bw. Gama aliwataka wahandisi kutumia elimu yao kubuni kulingana na mazingira na kwamba ni lazima ramani za ujenzi ziende na tahadhari ili kuepuka madhara na hasara hapo baadae.

“Mnasema jengo hili limejenga hivi kwa sababu ni la wasichana, lakini si sahihi kwani hata kama mnazuia wasichana kutoroka ni lazima muangalie namna ya kuwadhibiti, kwani haiwezekani kuziba jengo lote hivi kwa kuhofia wasichana kutoroka, hii ni hatari sana ni lazima majengo kama haya yajengwe kwa tahadhari,” alisema Bw. Gama.

Awali akizungumza mhandisi wa halmashauri ya wilaya ya Moshi Injinia Joab Mutagabwa, alisema Jengo hilo la bweni ambalo lilianza kujengwa septemba Mosi 2011 na kutarajiwa kukamilika septemba Mosi 2012 litagharimu sh. Mil 78 hadi kukamilika na kwamba kwa sasa liko katika hatua za mwisho.

Naye mkuu wa shule ya Sekondari Muungano Bw. Lucas Nko, alimwambia mkuu wa mkoa kuwa, shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo tatizo la upatikanaji wa maji hali ambayo huwalazimu kununua maji ndoo 40 kila siku ambapo ndoo moja ni sh. 300.