EAC yaomba muda zaidi kuzijadili Sudan na Somalia

Nembo ya EAC

By James Gashumba, EANA, Arusha

NCHI wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zitaendelea kufanya mashauriano zaidi juu ya maombi ya nchi mbili za Sudani Kusini na Somalia kutaka kujiunga na jumuiya hiyo yenye wanachama watano.

Uamuzi huo ulifikiwa mwishoni mwa mkutano wa Baraza la Mawaziri la EAC, ambalo ni chombo cha Sera cha Jumuiya hiyo, mjini Bujumbura nchini Burundi.

Vyanzo kadhaa kutoka katika mkutano huo vililiambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) kuwa Baraza lilikuwa na maoni kwamba maombi ya nchi hizo mbili ambayo yaliwasilishwa mwaka jana na mapema mwaka huu yanahitaji muda zaidi ili yaweze kufikiriwa na jumuiya hiyo ya nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

“Baadhi ya nchi wanachama zinahitaji muda zaidi kujadiliana na wadau wote kuhusu taarifa za kamati za uhakiki juu ya maombi ya Sudani Kusini,” vyanzo hivyo vimesema.

Ilikubaliwa kuwa taarifa ya timu ya wahakiki iliyotumwa Juba mwezi Julai kutathmini matayarisho ya Sudani Kusini kujiunga na EAC itawasilishwa katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri mjini Nairobi,Kenya, Novemba mwaka huu.

Kuhusu maombi ya Somalia, mawaziri hao walibainisha kuwa jambo hilo linahitaji majadiliano ya ziada na wadau zaidi wa kimataifa wanaojihusisha na juhudi za kuleta amani nchini Somalia.

Hata hivyo, Baraza lilimwelekeza Katibu Mkuu wa EAC kuwasilisha maombi ya Mogadishu katika kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama.