*Yasema kiwango cha umasikini Tanzania kinatisha
Na Joachim Mushi
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye kuacha
kuwatupia lawama Jeshi la Polisi nchini juu ya nguvu zaidi waliyoitumia katika
kukabiliana na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maeneleo (CHADEMA) mkoani Iringa,
ambapo yalisababisha kifo cha mwandishi wa habari Daud Mwangosi.
Kauli ya CUF imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Mkurugenzi Habari na
Uenezi, Mfumo Kambaya alipokuwa akihutubia wanachama wa chama hicho katika mkutano
wao mkubwa uliofanyika kwenye Viwanja vya Jangwani.
Katika mazungumzo yake Kambaya alisema anamshangaa Sumaye kuonekana anasikitishwa na
hatua ya Jeshi la Polisi juu ya matumizi ya nguvu ambayo inadaiwa ndiyo chanzo cha
mauaji ya mwanahabari (Mwangosi) wa Kituo cha Channel 10 Iringa, kwani tabia hiyo
aliwafundisha polisi tangu alipokuwa madarakani yeye kama Waziri Mkuu.
“..Mini namshangaa sana Sumaye kuonekana ameumia sana na tukio linalodaiwa polisi
kutumia nguvu na kusababisha mauaji ya Mwangosi, yeye apaswi kulalamika maana ndiye
aliyewafundisha kuua…tumeuliwa sana sisi na polisi kule Zanzibar, Mwembe Chai na
maeneo mengine kipindi yupo madarakani, sasa analalamika nini!,” alisema kiongozi
huyo wa CUF.
Hivi karibuni Sumaye alikaririwa na vyombo vya habari akionekana kutoridhishwa na
matumizi ya nguvu zaidi kwa Jeshi la Polisi katika kutimiza majukumu yake hali
inayodaiwa inasababisha vifo kwa baadhi ya raia.
Mkutano wa CUF ambalo ulikuwa maalumu kwa uzinduzi wa mikutano ya hadhara
inayotarajia kufanyika katika mikoa sita tofauti, ikiwa na kauli mbiu ya
“Mchakamchaka mpaka 2015” ambao umeudhuriwa na viongozi wa juu wa chama hicho kutoka
Tanzania Bara na Zanzibar ulihutubiwa pia na viongozi mbalimbali wa taifa wa chama
hicho.
Akizungumza katika mkutano huo Julias Mtatiro aliziponda kauli za baadhi ya viongozi
kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA kudai CUF ni chama cha kidini na
kuwaomba wananchi wawapuuze kwani hakuna hata siku moja chama hicho kilisilimisha
watu kwa imani tofauti.
Alisema kauli kama hizo ni hatua ya kuonekana kushindwa kueneza sera na kujikita
kwenye propaganda jambo ambalo halina msingi wowote. Alisema Serikali ya CCM
imeshindwa kuwatumikia wananchi wake na sasa watendaji wake wengi wamekalia kuwaibia
wananchi kila eneo, huku wakiendelea kutumia nguvu ya jeshi (mabomu na risasi) jambo
ambalo ni hatari.
“Iungeni CUF mkono maana sasa tunakwenda kuwangoa watendaji wa ‘wizi mtupu’ hii ni
mchakamchaka mkoa kwa mkoa hadi 2015,” alisema Mtatiro na kushangiliwa na umati wa
wana-CUF waliojitokeza katika viwanja hivyo.
Aidha kiongozi huyo alioneshwa kushangazwa na Tanzania kuonekana ikiomba misaada ya
vyandarua kutoka nje ya nchi kwa kutumia viongozi wake wa juu ilhali ina rasilimali
za kutosha kujitegemea.
Naye akizungumza na wana-CUF, Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema kwa sasa Tanzania ipo njia panda kwani hali ya maisha imepanda huku
idadi kubwa ya wananchi wakiwa hawana uwezo wa kumudu ugumu huo, jambo ambalo ni
hatari.
Alisema nchi ina rasilimali za kutosha na kama viongozi waliopo madarakani
(Serikali) wangezitumia vya kutosha na kuhakikisha zinamnufaisha kila Mtanzania hali
isingelikuwa kama ilivyuo sasa. “Nchi yetu ipo njia panda kwa sasa hali ya maisha
inatisha, watu wamegeuka ombaomba…CUF inasimamia haki sawa kwa wote hatuwezi
kukubali hali hii,” alisema Prof. Lipumba katika mkutano huo.
Alisema asilimia kubwa ya nchi ina ardhi yenye rutuba ambayo inakubali mazao mengi, achilia mbali madini mbalimbali ambayo yanapatikana kwenye ardhi ya Tanzania kama vile dhahabu, almasi, tanzanite na mengineyo. Jambo ambalo ni aibu kushindwa kuzitumia rasilimali hizo ikiwemo gesi inayochimbwa kwa sasa kuwanufaisha wananchi.
Hata hivyo kabla ya hotuba yake aliwaomba wananchi kukaa kimya kwa dakika moja kumkumbuka mwandishi Daud Mwangosi anayedaiwa kuuwawa kwa bomu katika mapambano ya Polisi wa kutuliza ghasia na wafuasi wa chama cha CHADEMA hivi karibuni mjini Iringa.
Kiongozi huyo pia alipokea kadi na magwanda kwa wananchi mbalimbali ambao walishawishika kujiunga na chama hicho, ambao wengi wametokea vyama vya CCM na CHADEMA.