Waziri wa Viwanda na Biashara ziarani mkoani Tanga

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Ukanda wa Uwekezaji wa Kiuchumi wa Mkoa wa Tanga, Chris Chae. Uwekezaji mkubwa unatarajiwa kuanza katika eneo hilo hivi karibuni.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda (Katikati), Mkuu wa Wilaya ya Tanga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Bi Halima Dendegu na watendaji wengine wa Mkoa wa Tanga wakipokea taarifa ya hali ya mgodi wa malighafi za kuzalisha saruji ya Lime stone unaomilikiwa na kiwanda cha Saruji Tanga.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda anafanya ziara ya siku tatu mkoani Tanga ikiwa ni maalumu kutembelea Viwanda na kuangalia utendaji wake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kutoka kitengo cha Habari na Mahusiano cha Viwanda na Biashara, ziara hiyo ni maalumu kwa lengo la kuvitembelea viwanda mbalimbali vya mkoa huo na kujionea utendaji wake, ikiwa ni pamoja na kuhimiza utendaji zaidi kwa sekta hiyo yenye mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi, ajira na pato la Taifa.
Taarifa zinabainisha siku ya kwanza ya ziara hiyo, Dk. Kigoda ametembelea Viwanda vya Saruji Tanga na Athi River, Kiwanda cha mifuko na maturubai cha Pee Pee, Kiwanda cha Unga wa ngano cha Pembe na Ukanda huru wa Uwekezaji Kiuchumi wa Mkoa wa Tanga.
Akizungumza katika maeneo yote, Waziri Kigoda amesifu juhudi za Uongozi wa Mkoa wa Tanga katika kufufua Viwanda vya zamani, kuibua fursa zilizopo katika sekta hiyo kwa kuanzisha Viwanda vipya pamoja na kampeni kubwa ya kuhimiza uwekezaji inayofanywa na mkoa huo.
Hata hivyo ameahidi jitihada zaidi zinafanywa na serikali katika kuongeza ufanisi wa sekta za Nishati hasa upatikanaji wa gesi na Umeme, miundo mbinu ya barabara, reli na bandari na ushiriki wa asasi za fedha katika kutoa mitaji ili kuisaidia sekta ya Viwanda kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi.
Ziara hiyo ya Waziri Kigoda na wasaidizi wake kutoka wizarani inaendelea Jumapili hii kwa kutembelea viwanda vingine mbalimbali.