Kangoye azungumzia maendeleo ya Benki ya Vijana

Wananchi wa Kijiji cha Msagali, Mpwapwa mkoani Dodoma, wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya TAYODA, Jackson Kangoye (hayipo pichani) alipokuwa akizungumza nao juzi na kuwahamasisha kujiingiza kwenye kilimo.

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Tanzania Youth Development Agenda (TAYODA), imesema mchakato wake wa kuanzisha benki ya vijana kwa lengo la kuwakomboa na kupata mikopo kupitia benki hiyo, unaendelea na upo kwenye hatua nzuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAYODA, Jackson Kangoye, alisema hayo juzi wakati akizungumza na baadhi ya vikundi vya vijana wilayani Mpwapwa, Dodoma ambao wamekuwa wakiwezeshwa na taasisi hiyo kufanya shughuli za kilimo na ufugaji.

Alisema taaratibu za kuanzisha benki hiyo zimeanza na wameshafikia hatua mzuri na wanasubiri hatua za kitaalamu kuanza maandalizi ya kuifungua.

Kangoye, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Bara. alisema lengo la kuanzishwa benki hiyo ni kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata mikopo kupitia benki yao badala ya kutumia benki zingine.

“Vijana wenzangu, taasisi yetu iko mbioni kuanzisha benki ya vijana, itakuwa mahususi kwetu na hivi sasa tumekutana na wataalamu wa masuala ya kibenki ambao watatushauri jinsi ya kuiendesha,” alisema.

Alisema baada ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa masuala ya kibenki, watakutana na baadhi ya vijana kuangali namna ya kuiendesha benki hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya vijana, walisema wamefurahishwa na uamuzi huo na wamewaomba viongozi wa taasisi hiyo kuhakikisha benki hiyo inafunguliwa kwa wakati. Said Husein, mkazi wa Kibakwe, alisema kuanzishwa kwa benki hiyo kutawakomboa vijana wengi ambao watakuwa wakipata mikopo kupitia benki hiyo.