BAADHI ya Waumini wa Kiislamu jijini Dar es Salaam leo wameandamana kuelekea makao makuu ya Jeshi la Polisi nchini ikiwa ni hatua ya kushinikiza wenzano waliokamatwa maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa tuhuma za kupinga zoezi la sensa ya watu na makazi iliyofanyika hivi karibuni nchini Tanzania.
Waumini hao wakiwa na mambango mbalimbali waliandamana na kuishia katika jengo la makao makuu ya polisi lililopo katikati ya jiji la Dar es Salaam ambapo walipofika hapo waliombwa kutoa wawakilishi wao ambao walikutana kwa mazungumzo na baadhi ya maofisa wa jeshi kuwasikiliza kilio chao.
Hata hivyo baada ya mazungumzo walitoka na ujumbe ambao waliutoa kwa waumini wenzao kuwa Jeshi la Polisi Nchini limekubali kuwaachia watuhumiwa wote waliokamatwa wakipinga sensa hivi karibuni maeneo mbalimbali ya Tanzania. “Tumekubaliana kuwa kuanzia sasa Jeshi la Polisi litawaachia wananchi wote waliokamatwa kwa tuhuma za kuwashinikiza wenzao wasiesabiwe katika sensa ya watu na makazi,” alisema mmoja wa viongozi mara baada ya kutoka kwenye mazungumzo na maofisa wa polisi.
Waumini hao kwa pamoja ilipofika muda wa Swala ya Ijumaa walifanya ibada yao hapo hapo nje ya Jengo la Makao Makuu ya Polisi kwa utulivu mkubwa. Katika maandamano hayo licha ya vikosi vya kutuliza ghasia na askari kuwepo hakuna nguvu yoyote iliyotumika kuwatawanya waumini hao.