Kikwete apewa tuzo Maalum ya Sera za Usalama wa Chakula na Uongozi

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikabidhiwa Tuzo ya Uongozi Bora wa sera ya Kilimo na Chakula toka kwa Bw. Ajay Vashee, Makamu Mwenyekiti wa asasi isiyo ya kiserikali inayohusika na sera za kilimo na chakula na Maliasili n ijulikanayo kama Food, Agriculture and Natural Resources Policy (FANRPAN) katika hoteli ya White Sands jana Septemba 5, 2012. Anayeshuhudia kulia ni Katibu Mtendaji wa FANRPAN) Dk Lindiwe Sibanda. Tuzo hiyo, ambayo hutolewa kwa kiongozi aliyefanya juhudi kuhakikisha kuwepo kwa sera bora za kilimo na chakula nchini kwake, ilichukuliwa na Malkia Ntombi Indlovukazi wa Swaziland mwaka jana, wakati Rais Hifikepunye Pohamba alitunukiwa mwaka 2010, Rais Armando Emilio Gwebuza mwaka 2009 na Rais wa Malawi, Hayati Bingu Wa Mutharika, aliipokea mwaka 2008. Picha na Ikulu.

Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ametunukiwa Tuzo Maalum ya Sera za Usalama wa Chakula na Uongozi Katika Sekta ya Kilimo ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wake na uongozi wake katika sekta hiyo ya kilimo.
Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya Mtandao wa Kutathmini Sera za Kilimo na Maliasili – Agriculture and Natural Resources Policy Analysis Network (FANRPAN) katika hafla maalum iliyofanyika jioni ya jana, Jumatano, Septemba 5, 2012, wakati wa mkutano wake wa mwaka unaofanyika kwenye Hoteli ya White Sands mjini Dar es Salaam.
Rais Kikwete anakuwa kiongozi wa tano wa Afrika kupokea Tuzo hiyo ambayo kwa lugha ya Kiingereza inajulikana kama Food Security Policy Leadership Award tokea kuanzishwa kwa Tuzo hiyo mwaka 2008 wakati ilipotolewa kwa aliyekuwa Rais wa Malawi, Hayati Bingu Wa Mutharika.
Viongozi wengine ambao wamepata kutunukiwa Tuzo hiyo ni Rais Armando Emilio Guebuza wa Mozambique mwaka 2009, Rais Hifikepunye Pohamba wa Nambia mwaka 2010 na Malkia, Mama wa Mfalme Ntombi, Indlovukazi wa Swaziland.
Mkutano huo wa mwaka wa FANRPAN unahudhuriwa na wajumbe 249 kutoka nchi 23 zikiwamo 16 ambazo ni wanachama wa taasisi hiyo ambazo ni pamoja na Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Mauritius, Mozambique, Kenya, Madagascar, Malawi, Namibia, Swaziland, Afrika Kusini, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Akizumgumza kabla ya Rais Kikwete kukabidhiwa Tuzo hiyo, Mtendaji Mkuu wa FANRPAN, Dk. Lindiwe Majele Sibanda alimwelezea Rais Kikwete kuwa ni bingwa mtetezi na kiongozi shupavu wa sekta ya kilimo katika Tanzania na Barani Afrika.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiangalia baadhi ya ng’ombe anaowafuga kwa kufuata njia za kisasa kwenye shamba lake kijijini kwake Msoga, Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, leo Septemba 6, 2012. Picha na Ikulu.


Alisema mama huyo: “Mheshimiwa Rais wewe ni bingwa. Unatanguliza mahitaji ya watu wako mbele kama vile unavyofanya katika sekta ya kilimo ambayo ni tegemeo la watu wengi katika Tanzania na Bara letu. Kupitia mipango yako ya kilimo, kamwe Tanzania haitakuwa ile ile ambayo uongozi wake uliupokea mwaka 2005. Kamwe Tanzania imebadilika sana chini ya uongozi wako.”
Dk. Sibanda aliongeza: “Kwa hakika umefanya mengi siyo kwenye kilimo tu, bali kwenye kusimamia amani na usalama, katika kukuza uhuru wa kila aina, katika masuala ya afya, elimu, miundombinu na maendeleo ya vijana.”
Hata hivyo, Dk. Sibanda alitoa changamoto tatu kwa Rais Kikwete ambazo ni kumtaka aongeze maradufu matumizi ya mbolea kwa wakulima kutoka kilimo kilo 10 za sasa kwa hekta moja hadi kufikia kilo 25 ifikapo mwaka 2015.
Aidha alimtaka Rais Kikwete kuhakikisha kuwa anaongeza maradufu uzalishaji wa mazao ya kilimo na hasa kuhakikisha kuwa Tanzania inajitosheleza kwa sukari ifikapo mwaka 2015 na tatu kuwashirikisha wakulima wadogo katika uzalishaji mbegu. “Tutarudi tena Mheshimiwa Rais mwaka 2015 kuyatazama tena upya mambo haya matatu.”
Akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo hiyo, Rais Kikwete aliwapitisha washiriki wa mkutano huo kwenye hatua zote ambazo Serikali yake inachukua kupambana na changamoto zote zinazokifanya kilimo cha Tanzania kubakia kwenye uduni ikiwa ni pamoja na kuongeza maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya mbegu bora, matumizi ya madawa ya kuua wadudu, matumizi ya mbolea nyingi zaidi, uboresha wa miundombinu ya barabara vijijini, uimarishaji wa vikundi vya ushirika wa uzalishaji na upanuzi na uimarishaji wa masomo.
Aidha, Rais aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali yake iko mbioni kuanzisha Soko la Mazao (Commodity Exchange) kama namna ya kuwawezesha kwa uhakika wakulima kwa kuhakikisha wanapata bei nzuri ya mazao yao.