RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Septemba Mosi, 2012, ameaga mwili wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi ambaye alifariki dunia usiku wa Agosti 20, mwaka huu.
Rais Kikwete ambaye aliwasili mjini Addis Ababa mchana wa jana kushiriki mazishi ya Meles Zenawi yanayofanyika Jumapili, 2 Septemba, 2012. Ameuaga mwili wa Meles Zenawi kwenye Kasri ya Waziri Mkuu.
Rais Kikwete ambaye msafara wake ni pamoja na Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Waziri Mkuu na ambaye kwa miaka 10 alikuwa Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliokuwa na makao makuu yake mjini Addis Ababa aliwasili kwenye Kasri ya Waziri Mkuu kiasi cha saa 10 na dakika 35 mchana na kwenda moja kwa moja kutia saini kwenye kitabu cha maombolezo.
Baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo, Rais Kikwete aliweka shada la maua kwenye jeneza la mwili wa Meles Zenawi na baadaye akaijulia hali na kuipa pole familia ya Meles Zenawi akiwamo mjane wa marehemu, Mama Azeb Mesfin ambaye alipigana msituni pamoja na Meles Zenawi na pia ni Mbunge katika Bunge la Ethiopia.
Mbali na Salim Ahmed Salim, ujumbe wa Tanzania kwenye mazishi ya kiongozi huyo unawashirikisha waliopata kuwa mabalozi wa Tanzania katika Ethiopia Jenerali Sam Hagai Mirisho Sarakikya na Christopher Liundi. Wengine katika msafara huo ni Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Haroub Ali Suleiman na wabunge
Livingstone Lusinde (CCM-Mtera) na Zitto Kabwe (Chadema – Kigoma Kaskazini). Rais Kikwete alimfuatia Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Rais Boni Yayi wa Benin na yeye akafuatiwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda katika kuuaga mwili wa Meles Zenawi.
Akizungumza na waandishi wa habari wa kimataifa mara baada ya kusalimiana na familia ya Meles, Rais Kikwete amemwelezea kiongozi huyo wa Ethiopia kama “mtu mkweli ambaye katika maisha hakusita kusema jambo aliloliamini.” Amesema Rais Kikwete: “Alikuwa kiongozi mwenye uwezo mkubwa.
Ucheshi wake, bongo yake, imani yake katika masuala makubwa ya maendeleo ni mambo yasiyokuwa rahisi kuyapata kwa viongozi wengi. Ni bahati mbaya sana amekufa akiwa mdogo”. Meles Zenawi amefariki akiwa na umri wa miaka 57 baada ya kuwa ameingia madarakani miaka 21 iliyopita wakati alipokamata madaraka ya urais kufuatia vita ya msituni.