Na Nicodemus Ikonko, EANA
KITUO cha Mafunzo Maalum Afrika (ACSS) kimeaandaa warsha ya wiki moja mjini Arusha, kujadili mbinu za Kupambana na Mitandao ya Uhalifu na Vitisho dhidi ya Usalama.
Warsha hiyo itajumuisha maafisa zaidi ya 50 waandamizi katika sekta ya usalama kutoka Afrika Mashariki, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Marekani kuongeza uelewa wa masuala ya usalama katika Afrika na kuona ni jinsi gani Marekani inaweza kuunga mkono kwa kujenga uwezo wa kupambana na usafirishaji wa madawa ya kulevya na ugaidi barani.
Kanda ya Afrika Mashariki hivi karibuni imekumbwa na vitisho mbalimbali vya usalama ikiwa ni pamoja na ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, madawa ya kulevya, wizi wa magari, umiliki haramu wa silaha na wizi katika mitandao.
Akihutubia mkutano uliomalizika hivi karibuni wa maafisa waandamizi wa masuala ya usalama katika nchi wanachama wa EAC mjini Kigali, Rwanda, Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Dk. Julius Rotich alibaini kuwa kanda hiyo ya Afrika imekuwa njia ya kupitishia madawa ya kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu, hali ambayo alisema lazima ikomeshwe mara moja kabla haijafikia pabaya.
Aliongeza: “Changamoto zinazotolewa na ugaidi, moja kati ya tishio kubwa katika kanda inasisitiza umuhumu wa sekta hii katika kuhakikisha kwamba watu wake wanasafiri kwa uhuru na salama. Suala hili lina umuhimu unafanana na vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu ambapo kanda hii inatumika kama njia kuu ya kupitishia,”
Warsha hiyo inayogharimiwa na Kamandi ya Marekani Afrika (AFRICOM) na Wakala wa Kudhibiti Vitisho dhidi ya Usalama (DTRA) inaratibiwa kwa pamoja na EAC na ACSS, matawi ya Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC.
Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera atahutubia wajumbe wa warsha hiyo wakati wa ufunguzi wake. Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso Lenhardt na Kaimu Mkurugenzi wa ACSS, Michael Garrison pia watakuwa miongoni mwa watakaozungumza katika warsha hiyo.