‘Serikali imeumia msiba wa Askofu Paschal Kikoti’

Askofu William Paschal Kikoti

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imefadhaishwa na msiba wa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Mhashamu Paschal William Kikoti ambao ulitokea kwa ghafla.

Waziri Mkuu ametoa salaam hizo Septemba Mosi, 2012 kwenye ibada ya mazishi ya Askofu iliyofanyika kwenye Kanisa la Mt. Maria Imakulata mjini Mpanda.

Mhashamu Askofu Kikoti alifariki dunia Agosti 28, mwaka huu katika Hospitali ya Bugando, jijini Mwanza amezikwa kwenye kanisa hilo ambalo ndiyo makao makuu ya Jimbo Katoliki Mpanda.

Waziri Mkuu alisema: “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wote wa Serikali kwa jumla, tumefadhaishwa sana na msiba huu mkubwa, tena uliotokea kwa ghafla. Lakini kwa kuwa haya ni mapenzi yake Mungu ambaye ndiye Muumba wetu sote tumelazimika kuipokea taarifa hii kwa majonzi makubwa.”

Alisema yeye binafsi alifarijika sana na uongozi wake, maono yake na shauku yake ya kutoa huduma za kiroho na za kijamii kwa jumla. Alisema mchango wake umegusa jamii nzima na siyo tu katika kutoa huduma za kiroho, bali pia huduma za kijamii zilizolenga kuleta maendeleo kwa wananchi katika Jimbo la Mpanda na nchini kote.

“Mhashamu Askofu Kikoti, ametutoka akiwa na umri mdogo sana wa kichungaji wa miaka 55, baada ya kulitumikia jimbo hili kwa miaka 11. Kabla ya kifo chake alikuwa na malengo mengi mazuri yakiwemo ya kufungua Seminari Ndogo ya Jimbo, kujenga Kituo cha Kichungaji na Kijamii na kupanua Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maria ya hapa Mpanda. Hivyo basi ni dhahiri kwamba kifo hiki ni pigo kubwa siyo kwangu, au kwa waumini wa Kanisa Katoliki, au Wanampanda tu, bali wananchi wote nchini kwa jumla,” alisema.

Mapema akitoa salaam za Baba Mtakatifu katika ibada hiyo ya mazishi, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Mhashamu Askofu Francisco Montecillo Padilla alisema hayati Baba Askofu Kikoti hatasahaulika kwa mema aliyoyatenda Iringa akiwa Padri na hapa Mpanda akiwa Askofu.

“Nilimfahamu Askofu Kikoti Februari, mwaka huu mara baada ya kuanza kazi hapa nchini… alikuwa ni mtu wa maneno machache lakini wa vitendo zaidi. Tunashukuru kwa kuijenga Dayosisi hii mpaka sasa, kuwajali watu wake na zaidi ya yote kuwapenda,” alisema.

Aliwasihi waumini wa Jimbo Katoliki la Mpanda kuendelea kuwa na umoja hasa katika kipindi hiki cha majonzi.

Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ilihudhuriwa na Maaskofu 28 kutoka majimbo mbalimbali ya Tanzania isipokuwa Askofu Renatus Msonganzila wa Musoma na Askofu Aloycius Balina wa Shinyanga ambao walitajwa kuwa ni wagonjwa. Maaskofu wa Mbulu na Moshi waliwakilishwa na wasaidizi wao.

Wakati huo huo, katika ibada hiyo ya mazishi, Askofu Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga alitangazwa rasmi kuwa ameteuliwa na Baba Mtakatifu Benedict wa 16 kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Mpanda hadi atakapotangazwa Askofu mwingine. Uteuzi wake umeanza Agosti 31, 2012.