TGNP yataka DC Korogwe awajibishwe kwa udhalilishaji

Mary Rusimbi (kushoto)akitetea jambo na Mkurugenzi wa TGNP, Ussu Mallya

Na Joachim Mushi

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), umeitaka Tume ya maadili ya utumishi wa umma, na mamlaka nyingine za kinidhamu kumchukulia hatua za kinidhamu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Mrisho Gambo kufuatia kauli ya udhalilishaji aliyoitoa hivi karibuni kwa mwanasheria wa Halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya imesema mtandao huo umesikitishwa sana na kauli iliyotolewa na Gambo, kwa mwanasheria wa Halmashauri hiyo Bi. Najum Tekka, kuhusu uhalali wa shahada yake ya uanasheria.

“Kauli hii ni udhalilishaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za wanawake na inaenda kinyume na misingi ya kuzingatia usawa sanjari na Katiba ya nchi; Uwezeshaji wa wanawake na utekelezaji wa Maazimio ya Haki na Usawa katika ngazi za Kimataifa Kikanda na Nchini Tanzania,” ilisema taarifa ya TGNP.

Aidha TGNP ilisema kauli hiyo imelenga kupotosha na kukatisha tamaa juhudi kubwa wanazofanya wanawake na wasichana katika kupata elimu na mafanikio mbalimbali nchini Tanzania.

Zaidi ya hapo, kauli hii inadhalilisha na kushusha hadhi ya vyuo vya elimu ya juu vinavyofanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa Watanzania.

“…Kauli iliyotolewa na Gambo, kwa mwanasheria wa Halmashauri hiyo Bi. Najum Tekka, kuhusu uhalali wa shahada yake aliyonayo hususan kuihusisha na vitendo vya ngono! Kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari ikiwepo gazeti la Majira Augosti 29,2012 Uk.3,”

Bi. Mallya alisema kutokana na kauli hiyo DC amekiuka maadili ya uongozi wa umma na kukidhalilisha kiti cha ukuu wa wilaya na kiongozi Mkuu wa nchi aliyemteua kushika wadhifa huo. Aidha kauli ya kiongozi huyo ya kutimia mahakama kutetea hoja yake, kunaashiria ubabe, ujeuri, vitisho, kiburi na dharau ya kutaka kuingilia uhuru wa mahakama na ajenda binafsi isiyokuwa na maslahi kwa wanawake na umma wa Watanzania.

“Kutokana na kauli hiyo ya udhalilishwaji, sisi wanaharakati wa ukombozi wa wanawake Kimapinduzi, usawa wa kijinsia, haki za kibinadamu demokrasia tunalaani vikali kauli za DC na kutoa Rai ifuatayo.”

Pamoja na hayo TGNP imemtaka Mkuu wa Wilaya Mrisho amwombe radhi Mwanasheria Bi. Najum Tekka, kwa kosa la kumdhalilisha kijinsia, Tume ya maadili ya utumishi wa umma, na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kutumia lugha ya kudhalilisha watumishi kinyume na maadili.

Aidha aliwataka wanawake wote, wanaume, vijana wa kike na kiume kuendelea na mapambano dhidi ya mfumo dume na mifumo yote kandamizi, kushikamana katika kudai misingi ya kisheria, uwajibikaji inayozingatia usawa na haki na kukataa kudhalilishwa katika ngazi binasfi na za umma.