Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Baba Askofu William Paschal Kikoti. Kifo cha Askofu Kikoti kimetokea Agosti 28, 2012 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mkoani Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu kutokana na ugonjwa wa Shinikizo la Damu.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Baba Askofu William Paschal Kikoti wa Jimbo Katoliki la Mpanda akiwa bado na umri mdogo wa miaka 55 wakati ndiyo kwanza utumishi wake ulikuwa ukihitajika zaidi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza.
“Ni dhahiri kwamba kifo cha Baba Askofu Kikoti kimeacha pengo kubwa la kiuongozi siyo tu kwa Kanisa Katoliki hapa nchini, bali pia Jumuiya ya Waamini wa Kanisa hilo kote duniani”.
Rais Kikwete amesema anatambua jitihada kubwa za Marehemu Baba Askofu William Paschal Kikoti enzi za uhai wake katika kuwatumikia Waumini wa Kanisa lake, na hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, tangu alipopata Daraja la Upadre mwaka 1988, kuteuliwa kwake kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda mwaka 2000, na hatimaye alipowekwa Wakfu na Kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo hilo mwaka 2001.
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Salamu zangu za Rambirambi, na kupitia kwako kwa Kanisa Katoliki na kwa Waumini wote wa Kanisa hilo hapa nchini hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, kwa kumpoteza mmoja wa Viongozi muhimu na wa ngazi ya juu wa kiroho, Marehemu Baba Askofu William Paschal Kikoti”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipumzishe mahala pema peponi Roho ya Marehemu. Amewahakikishia wote waliofikwa na msiba huo kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.