Uganda kuwa kituo cha rufaa uchunguzi wa vielelezo vya uhalifu EAC

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

Na James Gashumba, EANA-Arusha

MAWAZIRI wa masuala ya Usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamepitisha bila kupinga, Uganda kuwa mwenyeji wa Kituo cha Rufaa cha Kuchunguza Vielelezo vya Uhalifu (RFRC) vinavyohitajika katika kesi mbalimbali kwenye mahakama ndani ya kanda. Azimio hilo lilipitishwa mjini Kigali katika kikao cha siku moja kilichomalizika Jumatatu.

Hata hivyo, uamuzi huo unatakiwa kuthibitishwa na Baraza la Sekta ya Usalama linalojumuisha mawaziri wanaohusika na mambo ya ndani, shughuli za maafa, uhamiaji, polisi, magereza, intelijensia na udhibiti wa ugaidi.

Uamuzi wa umuhimu wa kupata kituo cha rRFRC ulifikiwa katika mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi katika nchi tano wanachama mjini Kigali uliomailizika Ijumaa iliyopita. Wakuu hao wa majeshi ya polisi waliunga mkono hatua hiyo baada ya kuzingatia taarifa ya utafiti ya ujumbe wa EAC uliotembelea nchi zote tano wanachama Machi mwaka huu.

Pia walizingatia taarifa ya kina ya uchunguzi huru wa mshauri wa uchunguzi wa vielelezo vinavyohitajika mahakamani kutoka Uingereza aliyekodiwa na EAC-GIZ na alishiriki katika ujumbe wa uthamini akiwa na wataalamu wa uchunguzi huo kutoka nchi za EAC.

Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera alisisitiza wakati akifungua mkutano wa mawaziri Jumatatu umuhimu wa ulinzi na usalama katika kanda.

“Wananchi Afrika Mashariki, mmoja mmoja na kwa ujumla wao wanategemea usalama wao kuimarika kwa vile utaratibu wa utangamano unaendelea kukua,” aliwaambia wajumbe.

Aliongeza: “Mategemeo ni kwamba tishio la ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na madawa ya kulevya pamoja na matishio mengine ya usalama yatadhibitiwa vyema na kwa njia rahisi,” Dk Sezibera alinukuliwa akisema, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EAC kwa waandishi wa habari.

Katibu huyo Mkuu wa EAC pia aliwapongeza Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa uamuzi wao kuanzisha kituo hicho cha rufaa cha uchunguzi.

Mwanyekiti wa Mkutano huo, Beatrice Kones kutoka Kenya alisema kuna haja kwa kanda kuwa na juhudi za pamoja kushughulikia tishio lolote la kiusalama.

“Bila amani, hakuna usalama na bila usalama hakuna maendeleo,” Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) nje ya mkutano huo.

Alisema pia kuwa RFRC itaanza shuguli zake muda mfupi ujao. Serikali ya Ujerumani imeonyesha nia ya dhati kuunga mkono uanzishwaji wa RFRC wa kisasa.