SUMATRA yang’aka kuhusu ajali

Moja ya ajali za magari

Na Waandishi wetu – MAELEZO

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imewataka wadau wa huduma za usafirishaji nchini kuzingatia kanuni na sheria za barabarani ili kupunguza ongezeko la ajali zinazotokana na makosa ya binadamu.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu, Ahmad Kilima amesema SUMATRA imekutana na wadau usafirishaji jijini Dar es Salam kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo pamoja na kupitia kanuni za leseni za usafirishaji kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekua tishio kwa maisha ya binadamu.

Amesema mamlaka hiyo imekutana na wadau hao kwa mujibu wa Kifungu namba 18 cha Sheria ya SUMATRA, 2001 kwa lengo lakutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo pamoja na kupitia kanuni na miongozo mbalimbali na nyenzo zinazosaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.

Aliongeza kuwa hivi sasa sekta ya usafirishaji nchini inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ongezeko la ajali za barabarani, miundombinu duni, msongamano wa magari hasa jijini Dar es salaam, uchafuzi wa mazingira na huduma duni zinazotolewa.

Alisema mkutano huo wa wadau ni muhimu katika maendeleo ya sekta ya usafirishaji nchini kwa kuwawezesha kujadili rasimu ya marekebisho ya kanuni za leseni za usafirishaji na namna ya kuzingatia vigezo vya ubora wa viwango vya huduma zinazotolewa na wadau hao na pia kupunguza ajali za barabarani ambazo asilimia 76 inasababishwa na uzembe wa madereva.

“Leo tutajadili Rasimu ya marekebisho ya Kanuni za Leseni ya Usafirishaji pamoja na Kanuni za Ufundi, Usalama na Ubora wa Viwango vya Huduma ili Kulinda maslahi ya watumiaji kwa Kulinda na kujenga mazingira ya kuvutia na kuhakikisha kuwa huduma za usafirishaji zinakidhi mahitaji,” amesema.

Ahmad amesema lengo kuu la kuzifanyia marekebisho kanuni hizo ni kuweka vifungu vitakavyotumika kama nyenzo muhimu katika kusimamia huduma ya usafirishaji kwa njia ya barabara ili huduma hiyo iwe bora na salama.

Aidha amewaeleza wadau hao kuwa maoni yao yatatumika katika kuboresha kanuni kwa kuingiza mapendekezo yao ambapo baada ya hatua hiyo ya awali rasimu ya kanuni hizo itawasilishwa Wizara ya Uchukuzi kwa kuihusisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili kanuni hizo zipitiwe ili ziweze kukidhi matakwa ya kisheria.

Kwa upande wake mwakilishi wa Chama Cha Kutetea Abiria nchini (CHAKUA) Bw. Wilson Mashaka ameiomba SUMATRA kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya usafiri ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na takwimu za abiria wanaotumia vyombo vyao ili iwe rahisi kujua idadi kamili ya abiria pindi vyombo hivyo vinapopata ajali ili kuondoa usumbufu unaotokea kwa ndugu wa abiria.

Pia amewataka wakaguzi wa SUMATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kushirikiana katika kuyakagua mabasi yanayobeba abiria na kuyachukulia hatua yale yasiyokidhi viwango vya kubeba abiria.

Naye mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji ya mabasi ya METRO Bw. Peter George ameitaka SUMATRA kwa kushirikiana na jeshi la polisi kuwachukulia hatua kali madereva wote wanaovunja sheria za usalama barabarani kwa kuendesha magari ya abiria kwa mwendo kasi ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukwa.