Na Hassan Abbas
MPANGO wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) umeungana na viongozi wa Bara la Afrika, wananchi wa Ethiopia na wabia wengine wa maendeleo ya Afrika kuomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa APRM makao makuu nchini Afrika Kusini na nakala yake kupatikana jijini Dar es Salaam, uongozi wa taasisi hiyo ambayo Zenawi alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Marais inayosimamia APRM, umeeleza kuwa kifo cha Zenawi kimeacha simanzi kuu na pengo katika uongozi wa mchakato huo.
“Jopo la Watu Mashuhuri la APRM limepokea kwa masikitiko na mstuko mkuu kifo cha Melesi Zenawi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ethiopia aliyekuwa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Marais na Viongozi wa Afrika wanaoiendesha APRM.
“Kwa niaba ya Jopo hili na Sekretarieti ya APRM makao makuu, na kwa niaba yangu binafsi, tunapenda kuwasilisha salamu za pole za familia ya APRM barani Afrika kwa Serikali na watu wa Ethiopia,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Jopo hilo, Prof. Amos Sawyer, Rais wa zamani wa Serikali ya mpito ya Liberia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, APRM imemueleza Zenawi, aliyekuwa kiongozi wa Kamati hiyo ya Marais tangu mwaka 2007 kuwa amechangia kwa kiasi kikubwa kuisukuma mbele taasisi hiyo ya kutathmini utawala bora barani Afrika ikiwa ni mapenzi yake kwa maendeleo ya watu wa Afrika.
“Kifo chake kimeacha huzuni na mstuko barani Afrika hasa wakati huu ambapo ameiacha APRM ikiwa taasisi inayokua kimajukumu na kiuongozi,” alisema Prof. Sawyer.
Akiwafariji wafiwa, Prof. Sawyer alisema Zenawi atakumbukwa kwa mema aliyoyafanya. “Katikati ya maombolezo haya, tunaamini familia yake na wadau wa APRM watafarijika na jambo moja kuu-mambo mema aliyoyatenda Zenawi wakati wa uhai wake,” imehitimisha taarifa hiyo.
APRM ni mchakato uliobuniwa na viongozi wa Bara la Afrika mwaka 2003 kwa nia ya kutathmini utawala bora katika kila nchi mwanachama kwa lengo la Afrika kujikosoa na kujisahihisha ili kuwaletea watu wake maendeleo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 kati ya 54 za Afrika zilizokwishajiunga moaka sasa na mchakato wa APRM na iko katika maandalizi ya kuwasilisha ripoti yake ya hali ya utawala bora kwenye kikao cha wakuu wa nchi za APRM cha Januari mwakani ili ijadiliwe na kupewa maoni ya kufanyiwa kazi.
Tayari Serikali ya Tanzania kupitia taarifa ya Rais Jakaya Kikwete imekwishatoa rambirabi kufuatia kifo hicho cha Zenawi aliyekuwa pia akiongoza programu kadhaa za Umoja wa Afrika ikiwemo NEPAD.