Mwanamke auawa kwa Imani za Kishirikina

Inspekta jenerali wa Polisi ,Said Mwema

Na Shomari Binda,Musoma

Mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Bibi Majira mkazi wa Kata ya Nyakato katika Manispaa ya Musoma ameuwawa na Wananchi wenye hasira kali kutokana na kutuhumiwa kushiriki katika Vitendo vya kishirikina.

Akizungumza na Mwandishi wa Habari hii jioni ya leo mara baada ya Tukio hilo lililotokea Mchana katika Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya hiyo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi Mwandamizi Absalom Mwakyoma amesema Mwanamke huyo alifariki Dunia mara baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya kupata Jeraha kubwa la panga katika upande wa kushuto wa Kichwa chake.

Kamanda Mwakyoma amesema Mwanamke huyo alivuja Damu nyingi baada ya kushambuliwa na Wananchi hao na hali yake ilikuwa mbaya zaidi mara baada ya kufikishwa katika Hospitali hiyo na alifariki baada ya muda mfupi.

Amesema si vyema kujichukulia sheria mikononi na kupoteza Uhai wa Binadamu kwa Imani za kishirikina na kusema Kitendo hicho ni kinyume cha Haki za Binadamu ambacho kinaweza kuleta Matatizo katika Jamii.

Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoani Mara amesema ajakipenda kitendo hicho na kukilani na kuitaka Jamii kubadilika na kujiepusha navyo kwani kunaweza kumuingiza Mhusika wa Matukio hayo katika Matatizo asiyoyategemea.

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kufatilia na litamfikisha katika Vyombo vya Sheria Mwananchi yeyote atakayebainika kuhusika katika tukio hilo ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Awali wakizungumza na Mwandishi wa Habari hii katika eneo la tukio hilo,Wananchi hao wa Kata ya Nyakato walisema wameamua kuchukua Sheria mkononi kutokana na kudai kuwepo kwa Matukio ya kishirikina katika Kata hiyo huku Serikali ikisema haitambui Imani za kichawi.