Nyumba 23 za wafugaji zachomwa na wakulima

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Said Mwema

Na Mwandishi wa Thehabari, Sumbawanga

MGOGORO baina ya wafugaji na wakulima umeibuka tena baada ya wakazi wa Kijiji cha Majalila wilayani Mpanda kuchoma moto nyumba 23 za wafugaji kwa madai mifugo yao imeharibu mazao katika mashamba ya wakulima.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tatu asubuhi katika Kijiji cha Majalila, baada ya wakazi hao wapatao 500 kuamua kuendesha msako kijijini hapo kwa lengo la kuwachomea nyumba wafugaji wa ng’ombe wanoishi kijijini hapo.

Katika tendo hilo la uchomaji wa nyumba za wafugaji zilizoezekwa kwa bati na nyasi kwenye baadhi ya nyumba zilitoka nyoka hali ambayo iliwafanya wakazi hao kuziua na kisha  kugawana vipande vipande kwa imani za kishirikina.

Habari zaidi kutoka Mpanda zinaeleza kuwa wananchi hao waliamua kuchukua sheria mkononi kwa kile walichokieleza uongozi wa Serikali ya Kijiji umeshindwa kuwachukulia hatua wafugaji hao kila wanapopelekewa malalamiko ya uharibifu wa mazao ya Mahindi na Tumbaku.

Inaelezwa kuwa polisi walipopata taarifa na kufika eneo la tukio wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Joseph Myovela na baadhi ya wajumbe wa ulinzi na usalama wa wilaya hiyo kwa lengo la kutuliza vurugu hizo. Viongozi hawa walijikuta kwenye wakati mgumu baada msafara wao kuzuiwa na wananchi waliokuwa na hasira huku wakiwa na silaha za jadi.

Hata hivyo polisi, waliweza kuwatuliza wakazi hao baada ya kuzungumza nao kwa muda mrefu na jazba iliposhuka wakakubali kufanya mkutano na viongozi wa wilaya. Akizungumza kwenye mkutano huo, Siadi Maninge ambaye ni mmoja wa wakulima alisema hali iliyotokea imekuja baada ya viongozi wa Serikali ya kijiji chao kushindwa kutatua mgogoro huo na kudaiwa kuwapokea wafugaji wenye makundi makubwa ya mifugo kijijini hapo bila kujali eneo lililopo halitoshelezi kwa kilimo na ufagaji.