CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepata pigo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, kutengua matokeo ya ubunge Jimbo la Igunga yaliyompa ushindi mgombea wake, Dk Dalaly Peter Kafumu.Dk Kafumu aliibuka mshindi katika uchaguzi mdogo uliofanyika Oktoba 2, mwaka jana kuziba nafasi ya Rostam Aziz ambaye alijiuzulu kwa madai kwamba anaachana na siasa chafu ndani ya CCM.
Uchaguzi huo ulikuwa wa ushindani mkubwa kati ya Dk Kafumu na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye ambaye hakuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo, hivyo kuamua kupinga matokeo hayo mahakamani. Kesi hiyo ilifunguliwa Machi 26, mwaka huu.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mary Nsimbo Shangali alisema Mahakama ilipokea malalamiko 15 ambayo yaliridhiwa na pande zote mbili, lakini baadaye yakaongezwa madai mengine mawili hivyo kufikia 17.
“Madai yaliyopokewa na Mahakama ni 17 na kati yake imethibitisha madai saba,” alisema Jaji Shangali katika hukumu hiyo.
Mbali na Dk Kafumu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uchaguzi walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga aliyetangaza matokeo hayo.
Dk Kafumu akizungumza na Radio One jana alisema tangu awali, hakuwa na imani na jaji aliyesikiliza kesi hiyo. Alisema hana mpango wa kukata rufaa, bali anawaachia viongozi wa CCM kufanya hilo.
Alisema baada ya ubunge wake kutenguliwa, anaendelea na shughuli zake za madini kwa kuwa ni mtaalamu wa sekta hiyo… “Ndugu mwandishi karibu Singida, mimi narudi kuendelea na shughuli zangu za madini.”
Sababu za kutengua matokeo
Alisema hoja zilizothibitishwa na Mahakama na ambazo zimetumika kutengua matokeo hayo ni pamoja madai kwamba Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alitumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbutu ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Igunga.
Dk Magufuli akiwa katika moja ya kampeni za uchaguzi huo, alitumia nafasi ya uwaziri kwa kuwatisha wapigakura wa jimbo hilo kwa kusema kama hawatamchagua mgombea wa CCM, watawekwa ndani.
Jaji Shangali aliendelea kueleza kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage alitangaza kuwa mgombea wa Chadema alikuwa amejitoa katika uchaguzi huo, jambo ambalo Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliokuwa ukitolewa.
Jaji Shangali alitaja hoja nyingine iliyotumika kufuta matokeo hayo kuwa ni kauli ya Imamu Swaleh Mohamed wa Msikiti wa Ijumaa Igunga, kuwatangazia waumini wa msikiti huo kuwa wasikichague Chadema, kwa kuwa baadhi ya viongozi wake wamemdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.Alisema hoja nyingine ni Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kudai kuwa Chadema kilileta makomandoo katika uchaguzi huo na kupanga kuuvuruga.
Hoja nyingine ambayo Jaji Shangali aliikubali ni ugawaji wa mahindi ya kuwawezesha wakazi wa Igunga kukabiliana na njaa wakati wa uchaguzi huo kwamba ulitumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kuwashawishi wananchi wawapigie kura.
Jaji huyo alihoji iwapo wakazi wa Jimbo la Igunga walikuwa na njaa sana wakati wa uchaguzi huo kiasi cha viongozi wa Serikali kuona kuwa ulikuwa wakati mwafaka wa kugawa mahindi hayo.
Kuhusu hoja ya upande wa utetezi kwamba mgombea wa Chadema, Kashindye alipaswa kupeleka malalamiko hayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alisema siyo ya msingi yanayoweza kumzuia mlalamikaji kupeleka malalamiko hayo katika Mahakama Kuu na hakuna kifungu chochote kinachomzuia mlalamikaji kufanya hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Shangali alisema kuanzia sasa Jimbo la Igunga lipo wazi na kwamba: “Milango iko wazi kwa walalamikiwa kukata rufaa ikiwa hawajaridhika na uamuzi.”
Hali ya usalama katika mahakama hiyo ilikuwa imeimarishwa, huku wafuasi wa Chadema wakiwa wengi zaidi na wakionekana kuwa na furaha hasa baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.
Dk Slaa, Nape wazungumza
Baada ya hukumu hiyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema: “Mahakama imedhihirisha yale ambayo tumekuwa tukisema kila wakati kwamba CCM inatumia mabavu.”
Alisema anashukuru Mahakama kwa kutoa haki na kukubaliana na Chadema kuwa CCM iligawa vyakula kwa wananchi ili kuwashawishi wawapigie kura.
-Kusoma zaidi habari hii tembelea http://www.mwananchi.co.tz