Wabunge wa CCM waibana Serikali kuhusu umeme

Pichani Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akizungumza jambo nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (Walemamvu) Mh. Al-Shaymaa Kwegyir mara baadaya kutoka kwenye kipindi cha maswali na majibu kwenye mkutano wa Nne wa Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012. Juni 8 ni siku ya kusomwa kwa Bajeti ya Serikali.   (Picha na Nicholaus Mmbaga-PMO)

Na Mwandishi Wetu, Thehabari, Dodoma

LICHA ya kuendelea kwa mgawo wa umeme unaozuka kila uchao, Serikali imesema imetumia dola za Marekani milioni 798 kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme tangu kipindi cha Awamu ya Pili hadi ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala (CCM) aliyetaka kujua Serikali imetumia kiasi gani cha fedha kuanzia kipindi cha Awamu ya Pili ya uongozi wa Serikali ya CCM kuzalisha umeme ilhali tatizo la mgawo linaendelea.

Kigwangala katika swali lake la msingi pia alitaka kujua tatizo la umeme nchini litaisha lini na kwa nini Serikali imekuwa hodari wa kupanga mipango mingi ya kutatua tatizo hilo bila kutekeleza.

Akijibu swali hilo Malima alisema kuwa tatizo la umeme litaisha baada ya kutekelezwa kwa kikamilifu na kwa wakati mpango wa kipindi kifupi cha mwaka 2011-2015.

Alibainisha kuwa miradi itakyotekelezwa katika kipindi hicho itaongeza jumla ya megawatt 1830 kwenye Grid ya Taifa kwa gharama inayokadiriwa Dola za Marekani milioni 3,700.

Akiuliza swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya aliitaka Serikali kutoa tamko rasmi la kumalizika kwa mgawo wa umeme kutokana na tatizo hilo kuwa sugu.

“Serikali itoe tamko rasmi la kumalizika kwa mgao wa umeme, maana ilishatangawa kumalizika kwa mgao huo lakini mpaka sasa kuna baadhi ya maeneo bado hakuna umeme, hili ni tatizo sugu Serikali ilitolee tamko,” alisema mbunge huyo.

Akijibu swali  hilo Malima alisema kuwa  ni vigumu kwa seriklai kutoa tamko hilo kutokana na kuwepo kwa upungufu wa megawatt 260 na kusema kuwa hata kama mitambo yote ikiwashwa bado kutakuwa na mgao wa umeme.