Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein,amewataka Wananchi kutowapa nafasi wasioitakia mema Zanzibar na badala yake wawajibike katika kufanikisha zoezi la sensa ambalo ni muhimu katika maendeleo nchini.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika Baraza la Idd El Fitri huko katika Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa inasikitisha kuwepo kwa baadhi ya Watu wanaowashawishi wenzao wasikubali kuhesabiwa kwa visingizio visivyokuwa na msingi.
Alisema kuwa mafundisho ya Dini zote hayapingi suala la kuhesabiwa kwa nia ya kupanga na kuleta Maendeleo ya Mwananchi na Nchi yake.
“Tunakumbuka kuwa Nchi yetu imeshafanya zoezi la Sensa kwa vipindi mbalimbali huko nyuma kwa ufanisi mkubwa bila ya kuwepo kisingizio chochote katika suala hili”,alisema Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa katika siku za hivi karibuni, Zanzibar ilikabiliwa na viashirio vya kuvunjika kwa Amani, Utulivu na Mshikamano na kusisitiza kuwa kuvurugika kwa amani ni jambo la muda mfupi lakini kuirudisha inachukua muda mrefu.
Alisema kuwa katika kipindi hicho yameshuhudiwa matukio mawili makubwa likiwemo lile la tarehe 26, 27 na 28 Mei na la 20 Julai Mwaka huu matukio ambayo yameitia Doa jamii ya Zanzibar ambayo imejijengea sifa nzuri pamoja na Amani na Utulivu.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa kuvunjia kwa Amani husababisha athari ya vitu na Watu wasio na hatia na kutoa wito kwa wananchi wote kuepuka vitendo vya uvunjaji wa Amani na vinavyopelekea kuathiri Watu na Mali zao.
Alieleza kuwa inapaswa kujua kuwa vitendo kama hivyo vinaathiri sana jitihada za Nchi katika shughuli za maendeleo na ukuaji wa Uchumi hasa katika kuimarisha sekta ya Utalii ambayo Serikali imeamua kuiimarisha kwa kauli mbiu’Utalii kwa wote’.
Dk. Shein aliitumia fursa hiyo kuwatanabaisha wanaopanga na kushabikia vitendo vya uvunjaji sheria, Amani na Utulivu kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wanaosababisha vurugu na kukiuka taratibu za Sheria.
Hata hivyo aliwasihi Wananchi kutojiingiza kwenye vitendo vinavyopelekea kuvunjika kwa Amani na badala yake wafanye mambo ya uadilifu yanayozingatia Sheria zilizopo na maadili yake ‘Tutumie busara katika kuyatatua matatizo yetu yanapotokea, kwa njia ya mazungumzo kwani hii ndio njia pekee…hakunalisilozungumzika”,
alisisitiza Dk. Shein.
Alisisitiza kuwa Serikali ina wajibu wa kulinda Haki na Uhuru wa Wananchi wake na Mali zao ambapo pia, Dk. Shein alilipongeza Jeshi la Polisi kwa mara nyengine tena kwa kazi nzuri walioifanya ya kutuliza Fujo zilizotokea.
Akieleza Mafanikio yaliopatikana kwa kipindi kifupi tangu muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Umoja wa Kitaifa ulipoanza, Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Alisema kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na viongozi na Wananchi kuishi kwa mashirikiano na kuvumiliana kisiasa ambapo kwa upande wa Serikali, Viongozi wamekuwa na Ushirikiano wa karibu na kuweza kufanya Kazi kwa misingi ya Katiba, sheria na kuheshimiana kwa manufaa ya Nchi.
Akizungumzia kuzama kwa meli ya MV Skagit, Dk. Shein alisema kuwa aliwataka Wananchi kumuomba Mola awalaze peponi wote waliopoteza Maisha katika Ajali hiyo na kueleza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kutokana Maafa hayo.
Katika kupunguza tatizo la usafiri wa baharini alieleza kuwa tayari ameshaipa maagizo Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuhakikisha kwamba katika kipindi cha miezi miwili ijayo wanakamilisha taratibu za kuagiza Meli mpya kubwa kwa ajili ya Abiria na Mizigo.
Alisema kuwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu katika kipindi cha miezi 15 ijayo inatarajiwa Meli hiyo kufika nchini, Meli ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba Abiria 1,000 Wananchi kuendeleza mafunzo waliyoyapata katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mapema asubuhi Dk. Shein aliungana na viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi katika sala ya Idd el Fitri huko katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Unguja na baada ya hapo alifika Ikulu mjini Zanzibar na kusalimiana na baadhi ya Masheikh, Makadhi na viongozi wengine wa Dini na Serikali.