Maafisa wa EAC wajadili Mbinu za kupambana na Uhalifu

Bendera ya Jumuia ya Afrika mashariki

Na James Gashumba

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa Dk. Julius Rotich ametaka kuwepo kwa juhudi za pamoja kudhibiti Wahalifu ambao wanaonekana kuleta shirikisho kati yao kwa haraka zaidi kuliko Nchi wanachama.

Alisema viwango vya Uhalifu kwa kutumia Mbinu za kisasa unazidi kuongezeka kutokana na nafasi nyingi za kujipatia Elimu huku kukiwa na tatizo la ukosefu wa Ajira.

‘’Changamoto hii inawataka nyinyi Wapelelezi kuendana na hali ya kuwa tayari kukabiliana nayo kwa kuimarisha uwezo wa Upelelezi ili kujihakikishia kwamba Wahalifu wanatiwa hatiani,’’ alisema.

Dk. Rotich alikuwa anahutubia mkutano wa Wakurungenzi wa Upelelezi, Wasajili wa Magari na Wakuu wa Vitengo vya Kupambana na Madawa ya Kulevya na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, mjini Nairobi, Kenya, mwishoni mwa wiki.

Alifafanua kwamba mahitaji ya hali ya juu ya Haki za binadamu na uwasilishaji wa Ushahidi ndani ya Kanda hiyo umeongeza shinikizo zaidi la kuwepo na nia ya kuimarisha uwezo wa kiufundi katika suala zima la upelelezi.

Ni kutokana na umuhimu huo basi, Sekretarieti ya EAC imeweka kipaumbele katika kuanzisha kituo cha uchunguzi cha kanda.

Alielezea Masikitiko yake kuhusu Taarifa za Wataalamu kwamba Wasafirishaji wa Madawa ya kulevya pamoja na Wasafirishaji haramu wa Binadamu wanatumia Kanda ya Afrika Mashariki kama Njia yao kuu ya kupitisha uhalifu huo.

Naye Mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Peter Kivuyo amezitaka Nchi wanachama kutoa adhabu kali zaidi kwa Wahalifu wa madawa ya kulevya.

‘’Hivi sasa Adhabu zinazotolewa kwa Wahalifu wa madawa ya kulevya au Mawakala wao siyo kali vya kutosha kuweza kuwaogopesha Watu wengine kutothubutu kujiingiza katika Biashara hiyo,’’ alisisitiza.

Akizungumza katika Mkutano huo pia, Mkuu wa Upelelezi nchini Rwanda, Christopher Bizimungu alisema ushirikiano waubadilishanaji wa Wahalifu wa madawa ya kulevya.

‘’Ushirikiano miongoni mwa Nchi wanachama wa EAC umeleta mafanikio katika kudhibiti uhalifu wa madawa ya kulevya katika kanda yetu.’’